Mwenyekiti wa tawi la CCM Moscow Dr. Alfred Kamuzola pamoja
na uongozi wote wa tawi kwa pamoja wameunga mkono kauli ya mwenyekiti wa CCM
taifa Dr. Jakaya Kikwete aliyoitoa juzi wakati akifunga mafunzo kwa watendani
na viongozi wa wilaya na mikoa wa Chama Cha Mapinduzi nchi nzima yaliyomalizika
huko Dodoma juzi tarehe 24 oktoba 2013.
Mwenyekiti wa chama taifa Dr. Jakaya Kikwete ameonesha
wasiwasi wake juu ya mafanikio ya chama katika uchaguzi wa serikali za mitaa
mwakani (2014) na katika uchaguzi mkuu ujao ( mwaka 2015) kutokana na vitendo
vya baadhi ya viongozi wa chama kutokuwa na maadili mema . Katika hotuba yake, Dr.Kikwete alisema, nukuu: “Kama hatutabadilika
katika suala la rushwa, mwaka 2015 tutakuwa na wakati mgumu sana, na
kama mwaka huo tutafanikiwa kuishika serikali, basi mwaka 2020 hatutarudi
tena madarakani…”.
“… Najua rushwa ipo
na mnaendelea kupokea sh laki mbili za ‘airtime’ (muda wa mawasiliano), ndugu
zangu hatutafika, ama wengine watavuka na wengine kukwama,” alisema.” Mwisho wa kunukuu.
Tawi linaunga mkono kauli hiyo kutokana na hali halisi kwamba
katika chaguzi zijazo, chama kitakuwa na wakati mgumu sana ili kushinda. Ni
lazima viongozi wabadilike kwa manufaa ya wanachama wao na watanzania wote. Mwenyekiti
wa chama taifa kaonesha kusikitishwa na hali ilipofikia ya baadhi ya viongozi
kufikia hatua ya kupokea rushwa kwa njia ya simu. Viongozi wa aina hiyo ni
lazima waachie ngazi na wawajibishwe.
Hata katika utendaji, viongozi wa vyama vya upinzani kwa sasa
wanafanya kila wawezavyo kukaa karibu na wananchi na kusikiliza shida kero zao
mara kwa mara. Wakati viongoziw walio wengi kwa upande wa chama chetu hawafanyi
vitu kama hivyo kwa kasi ambayo ingewavunja nguvu wapinzani. Lazima tujue kuwa
kila nafasi inayopatikana, wapinzani wanaitumia kwa nguvu zote ili kujiimarisha
hasa kwaajili ya chaguzi zijazo.
Kiongozi anapoonekana si muadilifu, basi ni lazima kuachia
ngazi na chama kumwajibisha kwa manufaa ya chama na kwa kufanya hivyo tutaweza
kujenga imani ya wanachama wetu. Kazi ya kujenga imani kwa wanachama ambao
wamechoshwa na matendo maovu ya baadhi ya viongozi ndani ya chama ni kazi ngumu
sana. Kwani ukishapoteza imani ya wanachama juhudi za
kurejesha imani yao kwa chama tena zinagharimu muda na rasilimali maradufu ili
angalau kuweza kurudisha imani ya wachache kati ya wengi ambao watakuwa
wamepoteza imani kwa chama.
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya watendaji na viongozi wa CCM ngazi za wilaya na mikoa hapa nchini, mjini Dodoma. |
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI.
No comments:
Post a Comment