Mheshimiwa Anne Makinda, Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Mizengo Pinda, Waziri Mkuu;
Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri;
Mheshimiwa Freeman Mbowe, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani
Bungeni;
Waheshimiwa Wabunge;
Mabibi na Mabwana;
Nakushukuru sana Mheshimiwa Spika kwa kukubali ombi langu na kutenga muda wenu
ili niweze kuzungumza na Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuhusu masuala muhimu kwa
uhai, ustawi na maendeleo ya nchi yetu na watu wake.
Mheshimiwa Spika;
Nimeambiwa kuwa taarifa ilipotolewa kuwa ninaomba kuja kuzungumza na Waheshimiwa
Wabunge, kumekuwepo na dhana mbalimbali. Wapo waliodhani kuwa nakuja
kuzungumzia mchakato wa kuunda Katiba mpya na hasa matukio ya wiki chache
zilizopita. Wapo waliodhani nakuja kuzungumzia “Operesheni
Tokomeza”. Tena wapo waliokwenda mbali na kufikiria kuwa nakuja
kuwakaripia Waheshimiwa Wabunge waliotoa maoni yao kuelezea kasoro
zilizojitokeza katika utekelezaji wa Operesheni hii muhimu. Na wapo pia
waliodhani ninakuja kuzungumzia ushiriki wa majeshi yetu ya Tanzania katika
Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa nchini Kongo.
Mheshimiwa Spika;
Hayo
si makusudio yangu. Kinachonileta mbele ya Bunge lako Tukufu ni
kuzungumzia Jumuiya ya Afrika Mashariki na mustakabali wa Tanzania katika
Jumuiya hiyo. Lakini, kwa sababu ya umuhimu wa masuala hayo niliyoyataja
na rai niliyopewa kuwa niyasemee japo kidogo. Nimeona ni vyema nifanye
hivyo.
Mheshimiwa Spika;
Kuhusu mchakato wa Katiba mpya, napenda kusema kuwa
tumefikia hatua nzuri katika utekelezaji wake. Kama mjuavyo Tume ya
Mabadiliko ya Katiba imekamilisha, kwa mafanikio, hatua ya mwanzo ya kusikiliza
maoni ya wananchi kuhusu Katiba wanayoitaka. Pia walishatoa Rasimu ya
Kwanza ya Katiba na kukamilisha mchakato wa Mabaraza ya Katiba.
Kinachosubiriwa kwa hamu na sisi wote, ni Rasimu ya Pili ya Katiba ambayo
inatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 15 Desemba 2013 au kabla ya hapo.
Mheshimiwa Spika;
Kwa
upande wa Bunge lako Tukufu, tunategemea kupata mambo mawili kutoka kwenu
yatakayowezesha mchakato kutekelezwa vizuri katika hatua zinazofuata.
Jambo la kwanza ni kutungwa kwa Sheria ya Kura ya Maoni na pili kufanyika kwa
marekebisho ya nyongeza ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu Bunge Maalum
ili kuboresha utekelezaji wake. Baada ya Bunge kukamilisha kazi yake hiyo
itafuatia uteuzi wa Wajumbe wa Bunge Maalum ili kazi ya kujadili Rasimu ya Pili
ya Katiba ifanyike na kutupatia Rasimu ya Mwisho. Rasimu ambayo ikikubaliwa na
wananchi katika Kura ya Maoni itakayofanyika wakati wo wote mwakani, tutakuwa
tumepata Katiba Mpya. Hivi sasa katika Serikali tunaendelea kufanya
tafakuri na tunachukua hatua za kuwezesha Bunge Maalum na Kura ya Maoni
kufanyika kwa mafanikio.
Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika;
Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuwa
sikukasirishwa na maoni yao kuhusu madai ya kuwepo kasoro katika utekelezaji wa
Operesheni Tokomeza. Shabaha ya Operesheni hii ni kuokoa maliasili za misitu na
wanyamapori dhidi ya uvunaji haramu ambao umefikia kiwango kinachotishia
kutoweka kwa raslimali hizo. Kwa kweli hali inatisha. Miti
inakwisha na ndovu na faru wanaangamia.
Mheshimiwa Spika;
Wakati, tunapata Uhuru Tanzania ilikuwa na ndovu waliokadiriwa kuwa takribani 350,000.
Lakini, kwa sababu ya ujangili uliokithiri katika miaka ya 1970 na 1980 ilipofika
mwaka1989 kulikuwa na ndovu wapatao 55,000 tu. Ilipofikia
hali hiyo Serikali ikaanzisha Operesheni Uhai iliyohusisha Jeshi la Ulinzi na
kuongozwa na Meja Jenerali John Walden (ambaye sasa ni marehemu)
kuendesha mapambano dhidi ya majangili. Kutokana na hatua hiyo na uamuzi wa
Shirika linalosimamia biashara ya wanyama walioko kwenye hatari ya kutoweka
(CITES) kupiga marufuku biashara ya pembe za ndovu duniani, idadi ya ndovu
nchini iliongezeka na kufikia 110,000 mwaka 2009.
Tumewaomba Fankfurt Zoological Society ambao ni wabia wetu
katika uhifadhi wa wanyama pori kwa miaka mingi wafanye sensa maalum ya ndovu
katika Hifadhi ya Selous na kote nchini ili tujue hali halisi ikoje. Kazi
hiyo inaendelea hivi sasa.
Mheshimiwa Spika;
Baada ya mwaka 2009 kumezuka wimbi jipya,
tena la nguvu kubwa, la kuua ndovu na faru nchini na kwingineko katika Bara la
Afrika ambako wanyama hao wapo. Idadi kubwa ya meno ya ndovu
yaliyokamatwa na yanaoendelea kukamatwa nchini na kwingineko duniani
inathibitisha ukweli huo. Kwa mfano, kati ya mwaka 2010 na Septemba,
2013, hapa nchini, kwa jitihada zetu vipande 3,899 vya pembe za ndovu
vyenye uzito wa kilo 11,212 na vipande 22 vya pembe za
ndovu zilizochakatwa zenye uzito wa kilo 3,978vilikamatwa. Aidha,
katika kipindi hicho vipande 4,692 vya pembe za ndovu vilivyotokea
Tanzania vyenye uzito wa kilo 17,797vilikamatwa nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika;
Kama
nilivyokwisha sema hapo awali matatizo ya kuuawa kwa wingi kwa ndovu na faru
lipo pia katika nchi nyingine Afrika zenye wanyama hao. Nchi za
Gabon, Kenya, Afrika ya Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Uganda, Zimbabwe,
Zambia na nyinginezo nazo zinakabiliwa na matatizo kama yetu. Tatizo
limekuwa kubwa kiasi cha kuifanya Jumuiya ya Kimataifa kushtuka na kuamua
kuingilia kati kwa namna mbili. Kwanza kuunga mkono juhudi za uhifadhi wa
ndovu na faru katika nchi zenye wanyama hao. Na, pili, kuchukua hatua
thabiti kudhibiti biashara ya meno ya ndovu duniani. Ni ukweli ulio wazi
kuwa kama hakutakuwepo na wanunuzi wa meno ya ndovu na faru hakuna ndovu au
faru atakayeuawa.
Mheshimiwa Spika;
Kutokana na ukweli ulivyo uamuzi wetu wa kuendesha
Operesheni Tokomeza ni sahihi kabisa. Manufaa yaliyopatikana baada ya
Operesheni Uhai ya mwaka 1989 yanatupa imani kuwa na safari hii pia
tutafanikiwa. Tusipochukua hatua kama hii sasa ni sawa na kuwapa kibali
majangili waendelee kumaliza ndovu na faru nchini. Hakika wanyama hao
watakwisha. Itakuwa ni aibu kubwa kwetu na historia itatuhukumu vibaya.
Mheshimiwa Spika;
Tumeyasikia maelezo ya Wabunge kuhusu kasoro mbalimbali zilizojitokeza katika
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. Nawaahidi kuwa tutayafanyia
kazi. Serikali imeahirisha kwa muda Operesheni hii ili kujipa muda wa
kurekebisha kasoro hizo na kujipanga upya. Watendaji wasiokuwa waadilifu
na wale wasiokuwa waaminifu wataondolewa. Halikadhalika, kasoro za
kimfumo nazo zitasahihishwa ili tutakapoanza upya Operesheni itekelezwe kwa
mafanikio yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika;
Miongoni mwa mambo yaliyozungumzwa kwa uchungu ni ukamataji wa mifugo
iliyokutwa kwenye mapori ya hifadhi za wanyama na vitendo vibaya walivyofanyiwa
wenye mifugo na mifugo yenyewe. Narudia kusisitiza kuwa taarifa zote hizo
zitafanyiwa kazi na waliohusika watachukuliwa hatua zipasazo. Pamoja na
hayo, napenda kuwakumbusha ninyi watunga sheria wetu kuwa sheria ya hifadhi za
wanyamapori hairuhusu mifugo kuchungwa katika maeneo ya hifadhi.
Naomba tuwakumbushe wananchi tunaowaongoza wajiepushe na
kufanya hivyo. Ni uvunjifu wa Sheria za nchi. Naomba pia, wananchi
waelimishwe ili wajue kuwa wakifanya hivyo na kukutwa katika maeneo hayo na
mifugo yao kuna adhabu iliyotamkwa kwenye sheria. Hivyo tusiwalaumu
wala kuwaona maafisa wanyamapori kuwa ni watu wabaya. Wanatekeleza Sheria
iliyotungwa na Bunge hili. Pale wanapotenda visivyo tuseme,
watawajibishwa ipasavyo.
Jeshi la Umoja wa Mataifa Kongo
Mheshimiwa Spika;
Mapema mwaka huu (2013) Umoja wa Mataifa uliomba nchi yetu ichangie kikosi
kimoja cha wanajeshi katika Brigedi Maalum iliyoundwa na Umoja huo kuongeza
nguvu ya kudhibiti waasi Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Lengo la msingi ni kuiwezesha nchi hiyo kupata amani ya kudumu ambayo
imekosekana kwa muda mrefu kutokana na kuibuka kwa uasi mara kwa mara.
Mheshimiwa Spika;
Mheshimiwa Spika;
Aina ya pili ni ile ya majeshi yanayopelekwa mahali ambapo
hakuna amani hivyo wanapewa jukumu la kuchukua hatua za kufanya amani
ipatikane. Majeshi haya hupewa mamlaka ya kutumia nguvu ya kijeshi dhidi
ya wanaosababisha amani ikosekane kama ni lazima kufanya hivyo. Maana
yake ni kwamba wanayo ruhusa kuingia katika mapigano dhidi ya watu au vikundi
vinavyovuruga amani. Tofauti na wenzao wa kundi la kwanza, wanajeshi wa
kundi la pili wako kwenye hatari zaidi ya kupoteza maisha au kujeruhiwa kuliko
wenzao ingawaje wapo wengi nao wameuawa na kujeruhiwa.
Mheshimiwa Spika;
Wanajeshi wetu wamekwenda Kongo chini ya utaratibu huu wa
pili ambao unahusu kuingia kwenye mapigano dhidi ya waasi kama hapana budi
kufanya hivyo. Wametekeleza majukumu yao vyema na kwa ujasiri
mkubwa na weledi wa hali ya juu. Bahati mbaya tumepoteza vijana wetu watatu
shupavu. Daima tutawakumbuka na tutawaenzi ipasavyo mashujaa wetu
hawa. Tuzidi kuwaombea kwa Mola awape mapumziko mema. Ameen.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii
kumpongeza Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa mafanikio
ya kihistoria waliyoyapata hivi majuzi dhidi ya waasi wa M23. Tunamtakia
yeye na wananchi wa Kongo kila la heri katika kazi ngumu iliyo mbele yao ya
kujenga upya eneo hilo na kujenga mahusiano mapya miongoni mwa watu wa
Kongo. Pia nawapongeza sana wanajeshi wa Brigedi Maalum ya Umoja wa
Mataifa kwa kazi nzuri waliyoifanya iliyowezesha mafanikio kupatikana.
Wanajeshi hao ni kutoka Afrika Kusini, Tanzania na Malawi wanaoongozwa na
Brigedia Jenerali James Aloisi Mwakibolwa wa JWTZ.
Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mheshimiwa Spika;
Mheshimiwa Spika;
Mheshimiwa Spika;
- Kujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Kampala, Kigali na Bujumbura.
- Ujenzi wa Bomba la Mafuta la kutoka Kenya hadi Uganda na Sudani ya Kusini.
- Kujenga Kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda.
- Kuanzisha Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutekeleza vipengele vyote;
- Kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki na kwamba itaundwa Kamati ya kuandaa rasimu ya Katiba ya Shirikisho.
- Kuharakisha uanzishwaji wa Visa ya pamoja ya Utalii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (Single East African Community Tourist Visa);
- Kuandaa utaratibu wa kutumia vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria katika nchi zao; na
- Kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme.
Mheshimiwa Spika;
Ni
dhahiri kwamba orodha hiyo imechanganya mambo yale ambayo ni ya Jumuiya na yale
yasiyo ya Jumuiya. Kwa mfano, mambo manne kati ya hayo manane hayamo
kwenye masharti ya kutokufanyika bila ya kuihusisha au kupata ridhaa ya Jumuiya
ya Afrika Mashariki. Jambo la kwanza ni uzalishaji na usambazaji wa
umeme. Ni kweli kwamba tunao mkakati wa kuwa na akiba ya pamoja ya nguvu
ya umeme (East African Power Pool). Hata hivyo, bado jukumu la kuzalisha
na kusambaza umeme huo limeachiwa nchi wanachama zenyewe kuamua. Lakini,
hivi ndugu zetu hawa wanao muhali kuishirikisha Tanzania katika mpango ambao
kimsingi umebuniwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo sote ni wanachama?
Jambo la pili, ni ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta
nchini Uganda. Hili si suala la Jumuiya bali la nchi ya Uganda kuamua
yenyewe peke yake au kwa kushirikiana na wadau wengine. Rais Yoweri
Museveni alituarifu mpango huo na sote tuliupokea kwa furaha kwamba sasa
tutapata mafuta karibu na nyumbani. Alitualika kushiriki katika
ujenzi wake sijui sasa amebadili mawazo kwamba Tanzania siyo muhimu.
Mheshimiwa Spika;
Jambo la tatu ni ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Kenya hadi
Sudani ya Kusini na Uganda. Hili si jambo linalobanwa na masharti ya
Jumuiya. Ni juu ya nchi hizi tatu kuamua kufanya ili kuwezesha mafuta yao
kufika kwenye masoko. Hata hivyo, nimeambiwa kuwa Jumuiya imeshazungumzia
bomba la mafuta kutoka Eldoret hadi Uganda, Rwanda na Burundi kuwa nalo lifike
Tanzania kupitia upande wa Kaskazini Magharibi mwa Tanzania. Inaelekea
mpango huo sasa haupo maana hatujausikia kutajwa katika ujenzi wa bomba hilo.
Mheshimiwa Spika;
Jambo la nne ni ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mombasa –
Kampala – Kigali – Bujumbura. Hili nalo hatuna tatizo nalo. Si
mradi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ni jambo lililo chini ya mamlaka ya nchi
wanachama husika. Hata hivyo, ni vyema kutambua ujenzi wa miundombinu ya
reli, barabara na usafiri wa anga na majini kuunganisha nchi za Afrika
Mashariki ni miongoni mwa mambo ya kipaumbele cha juu yanayoshughulikiwa na
Jumuiya yetu. Jumuiya hutengeneza mikakati ya pamoja na ndiyo maana tuna
East African Railway Masterplan, tuna East African Road Network, na tuna Lake
Victoria Development Programme kwa ziwa Victoria.
Kwa ajili hiyo, nilitegemea kuwa reli ya kutoka Mombasa hadi
Kigali na Juba ingekuwa na tawi linalounganisha reli hiyo na reli ya Tanzania
kama ilivyo reli ya Moshi – Voi – Taveta aliyotuachia mkoloni. Tulitegemea
hivyo kwa minajili ya kuunganisha soko la Afrika Mashariki ambapo naamini
Tanzania ni mdau muhimu. Lakini inaelekea kwa maoni ya wenzetu hivyo
sivyo.
Mheshimiwa Spika;
Lazima nikiri kuwa inashangaza na tunayo kila sababu ya
kuuliza kwa nini wenzetu wameamua kufanya hivi. Kumetokea nini toka
tukutane pale Arusha Aprili 28, 2013 na Juni 24, 2013 walipokutana kuamua
kufanya mambo ya kujenga na kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki kwa
kubaguana, Haijawahi kuwa hivi kabla.
Mheshimiwa Spika;
Katika mambo manne yaliyosalia ambayo yaliamuliwa na kuwekewa utaratibu wake wa
utekelezaji na Jumuiya ya Afrika Mashariki mawili hatuna maneno nayo.
Mambo hayo ni matumizi ya vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria na Visa
ya Pamoja ya Utalii kwani tuliamua kwa pamoja kuwa nchi wanachama zilizokuwa
tayari waanze. Lakini, kwa upande wa kuanzishwa kwa Himaya Moja ya Ushuru
wa Forodha (Single Customs Territory) na Shirikisho la Afrika Mashariki
tunadhani wenzetu wamekiuka uamuzi wetu wa pamoja.
Mheshimiwa Spika;
Mheshimiwa Spika;
Kutokana na uamuzi huo, Wakuu wa Nchi waliagiza Baraza la
Mawaziri kuunda Kikosi Kazi cha kujadiliana na kuandaa utaratibu wa utekelezaji
wa mfumo huo. Taarifa ya kikosi kazi inatakiwa kutolewa katika Mkutano wa
15 wa Wakuu wa Nchi utakaofanyika Kampala, Uganda tarehe 30 Novemba,
2013. Iweje leo nchi tatu wanachama ziamue peke yao kuanza
kutekeleza? Wanatekeleza nini na kwa nini wafanye hivyo?
Mheshimiwa Spika;
Mheshimiwa Spika;
Mheshimiwa Spika;
Mheshimiwa Spika;
Tunasikia eti kuwa baadhi yao walipoulizwa kwa nini wengine
hatupo wakasema kuwa wao wametangulia na sisi tutakapokuwa tayari
tutajiunga. Yaani wana Umoja wa Waliokuwa Tayari (Coalition of the
Willing). Hivi ni nani hayuko tayari (who is not willing?)
Haiwezekani watu waitane wenyewe bila ya kutualika halafu wadai kuwa wao ndiyo
wako tayari na kujenga dhana kuwa sisi wasiotualika ndiyo ambao hatuko
tayari. Madai hayo hayana ukweli. Ni vyema waseme ukweli.
Kama walitualika tukakataa ndiyo wanaweza kusema hayo.
Mheshimiwa Spika;
Kumekuwepo na madai kutoka kwa baadhi ya wenzetu, eti kwamba
Tanzania haina moyo wala dhamira ya dhati ya kuendeleza utengamano wa
Afrika Mashariki. Kwa sababu hiyo inasemekana eti nchi yetu imekuwa
kikwazo kwa maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba Tanzania tunawachelewesha
wengine kupiga hatua za haraka. Wanadai kama siyo hivyo Jumuiya ya Afrika
Mashariki ingekuwa mbali kwa maendeleo. Maneno hayo yamekuwa yanarudiwa au
kujirudia mara nyingi kiasi cha kuwafanya baadhi ya watu wa Afrika Mashariki na
hata kwingineko duniani waamini hivyo.
Mheshimiwa Spika;
Napenda kusema kwa dhati ya moyo wangu kwamba madai hayo
hayana ukweli wo wote. Isitoshe hata sababu zinazotolewa kuthibitisha
ukweli wake hazina mashiko. Hazifanani na ukweli kuhusu Tanzania na
Watanzania walivyo. Tanzania ni muumini wa dhati wa umoja na utengamano
wa nchi za Afrika Mashariki na Afrika. Tumethibitisha hivyo kwa vitendo
kwa kuunganisha nchi zetu mbili huru yaani Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na
Jamhuri ya Tanganyika na kuwa taifa moja liitwalo Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Muungano wa nchi zetu mbili ndio pekee uliodumu kwa muda mrefu
kuliko yote Afrika.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania ni mwanachama mwaminifu wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki kwa maana ya kutekeleza Mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo, kwa Itifaki
zake na maamuzi halali ya vikao na taasisi za Jumuiya. Kama lipo jambo
ambalo hatujalifanya ilivyotakiwa itakuwa ni kwa sababu za msingi na siyo kwa
sababu ya kupuuza Jumuiya. Tunaithamini sana Jumuiya na tumeipa kipaumbele cha
juu. Hatuwezi kuhangaika kwa gharama kubwa ya muda wetu, fedha zetu na
kutoa mchango wa hali na mali kuianzisha, kujenga na kuifikisha Jumuiya hapa
ilipo halafu tuwe ni watu tunaoongoza kutokuipenda na kudhoofisha maendeleo na
ustawi wake. Ni maneno ya kushangaza na wala hayaingii akilini. Ama kweli
akutukanae hakuchagulii tusi.
Mheshimiwa Spika;
Mheshimiwa Spika;
Tanzania imekuwa inawasihi wanachama wenzetu kuwa tujenge
Jumuiya yetu hatua moja baada ya nyingine kama ilivyo kwenye Mkataba
ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hatuna tatizo la kuongeza kasi
ya ujenzi wa Jumuiya lakini tusivuke hatua yo yote. Tusiende kasi ya
kupindukia. Mkataba unaelekeza tunaanza na Umoja wa Forodha, inafuatia Soko la
Pamoja kisha Umoja wa Kifedha na hatimaye Shirikisho la Kisiasa.
Mheshimiwa Spika;
Mheshimiwa Spika;
Mheshimiwa Spika;
Bila
ya shaka sote tutakumbuka kuwa mwaka 2006 Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya
waliunda Kamati Maalum katika kila nchi kukusanya maoni ya wananchi kuhusu
kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki. Kwa hapa nchini Kamati hiyo
iliongozwa na Profesa Samwel Wangwe na katika taarifa yake, Kamati
ilieleza kuwaasilimia 74.4 ya Watanzania wanaunga mkono kuwepo kwa
Shirikisho lakini ni asilimia 25.4 tu ndiyo waliunga mkono
kuharakishwa kwake.
Mheshimiwa Spika;
Mheshimiwa Spika;
Mheshimiwa Spika;
Mheshimiwa Spika;
Mheshimiwa Spika;
Nchi yetu inapenda kuona kuwa tunakuwa na Jumuiya ya Afrika
Mashariki iliyo imara na iliyo endelevu. Jumuiya ambayo inaendeshwa
vizuri, mambo yake ni mazuri na nchi zote wanachama na watu wake wananufaika
nayo, na hivyo wanaifurahia. Tanzania haina tatizo na kuharakisha
mchakato wa utengamano, lakini tunapata taabu kuruka baadhi ya hatua kabla
hazijakamilika. Tunawaomba wenzetu kuwa makini katika kila hatua
tunayochukua. Bila ya kufanya hivyo, Jumuiya yetu itakuwa
imejengeka katika msingi dhaifu hivyo ustawi na uhai wake utakuwa na changamoto
nyingi. Hatupendi ya mwaka 1977 yatokee tena.
Mheshimiwa Spika;
Tutaendelea kukumbushana umuhimu wa kufanya mambo
yanayojenga na kuepuka yale yanayoweza kubomoa. Tutakumbushana umuhimu wa
kuheshimu matakwa na masharti ya Mkataba ulioanzisha Jumuiya, Itifaki zake na
maamuzi halali ya vikao rasmi na asasi za Jumuiya. Tukifanya hivyo
Jumuiya ya Afrika ya Mashariki itadumu, itazidi kustawi na kunufaisha nchi
wanachama na watu wake kama yalivyo malengo na madhumuni ya kuundwa
kwake.
Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania
Idumu Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge;
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment