CHAMA CHA MAPINDUZI
UMOJA NI USHINDI, AMANI NA MAENDELEO ...!!!

Wednesday, November 6, 2013

RAIS JAKAYA KIKWETE KULIHUTUBIA BUNGE KESHO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete


Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muunguno wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, kesho mchana Novemba, 7 anatarajiwa kulihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma.

Habari kutoka Bungeni, Dodoma zinaeleza kuwa Mawaziri na Manaibu Waziri wote wameelekezwa kutokutoka nje ya Dodoma hadi hapo Mhe.Rais atakapokuwa amehutubia bunge. Pia safari zote za Kamati za Bunge ambazo zilikuwa zifanyike kesho zimeahirishwa hadi baada ya kesho ili kutoa fursa kwa wabunge wote kuwepo bungeni wakati wa hotuba hiyo.

Mara ya mwisho Mhe.Rais Kikwete alilihutubia Bunge Novemba 18, 2010 wakati wa ufunguzi wa Bunge la Kumi. Katika hotuba hiyo Rais Kikwete alielezea vipaumbele vya Serikali yake katika awamu ya pili ya uongozi wake.

Kati ya mambo ambayo yanatazamiwa kuongelewa na Mhe. Rais hapo kesho ni pamoja na mapendekezo ya marekebisho katika sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya 2013 ambayo ilipitishwa katika mkutano wa Bunge uliopita. Muswada huo ni matokeo ya majadiliano baina ya Serikali na Vyama vya siasa vyenye wabunge chini ya uratibu wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), baada ya vyama vya siasa kutoridhishwa na muswada uliokuwa umepitishwa katika mkutano wa bunge uliopita. 

Hii ni katika kujenga msingi wa maridhiano katika mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya kama ambavyo Rais Kikwete amekuwa akisisitiza mara kwa mara.

No comments: