CHAMA CHA MAPINDUZI
UMOJA NI USHINDI, AMANI NA MAENDELEO ...!!!

Friday, May 28, 2010

Taarifa kwa wanachama wa CCM Tawi la Moscow

SEHEMU YA I : 

 UTANGULIZI!!  Tafsiri sahihi ya Tawi
Tawi la Chama cha Mapinduzi nchini Urusi (CCM Moscow) linajumuisha wanachama wa CCM katika miji yote katika shirikisho la Urusi.

Tawi linaendesha shughuli zake katika misingi ya Uadilifu, uwajibikaji, heshima, ustahimilivu na Umoja kati ya wanachama wake kwa kuendeleza misingi ya Utawala bora , ikiwa ni pamoja na kuongeza uelewa wa siasa na historia ya chama kwa kufanya Mijadala mbalimbali kwa nafasi. Hii ni moja ya njia ya kukuza vipaji na uelewa wa vijana ili waweze kushika nafasi mbalimbali za Uongozi na utendaji katika chama na serikali.

Azimio la kuanzisha tawi hili , ilifikiwa Mwezi August 2008 kwa Tamko Rasmi, na hatimaye tarehe 3 /5/2009 ,Tawi Lilizinduliwa Rasmi na Mwenyekiti wa Muda Mhe. Dr. Alfred Kamuzora, Kwa Niaba ya kamati Kuu ya CCM, baada ya Kupata Utambulisho Rasmi toka Ofisi ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Nchini Tanzania.

Mpaka sasa Tawi la CCM  Moscow lina Jumla ya wanachama 87, ambao wengi wao walijiunga Rasmi na chama wakati wa sherehe za Uzinduzi  zilizofanyika Mwaka 2009.

KAULI  MBIU:
Kauli mbiu ya tawi , ni Kuandaa vijana na wanachama wa kudumu  wanaokulia katika Maadili ya CCM ya heshima, utashi , uwajibikaji na uadilifu na pia wenye mapenzi mema na chama.

Ambatanisho na hilo, nawasihi wanachama wote kufuatilia mwongozo wa Tawi na Katiba ya CCM, kufahamu hatua za utendaji,  kazi na malengo yake. Tafsiri hizi unaweza kuzipata kupitia website ya tawi ambayo ni:
www.ccmmoscow.blogspot.com , au wasiliana Moja kwa Moja na katibu na Utapewa Nakala zake.

SEHEMU YA II:

  MAFANIKIO,
Tawi  la CCM Moscow , toka kuzinduliwa kwake rasmi, tarehe 3/5/2009, limepata Mafanikio kama ifuatavyo:

(1)   Kupata Utambulisho toka Makao makuu na Kujumuishwa kuwa ni moja ya Matawi rasmi ya CCM nje ya ya Tanzania, ikifuatiwa na Uingereza , na Marekani. Hivyo kushirikiana Moja kwa Moja na ofisi ya Katibu Mkuu kwa Taarifa za Kiutendaji na Maelekezo ya Vikao Husika vya Kamati kuu na Halimashauri kuu .

(2)   Kufanikiwa kupata kadi za Uanachama wa  CCM  na UVCCM  , pamoja na kopy za vitabu za kiada na ziada vya chama, katiba ya CCM toleo la mwaka 2007, Kanuni za Mwongozo wa UVCCM. Picha  3 za mwenyekiti wa CCM Mhe. Raisi Jakaya Mrisho Kikwete  pamoja na picha za Wajumbe wa kamati kuu.

(3)   Kufanikiwa  kugawa kadi za CCM kwa wanachama wapya, Mnamo tarehe 3/5/2009, ambapo jumla ya kadi 74 ziligawiwa na Ongezeko kuendelea kwa kutokana Mahitaji ya Mkereketwa husika, Mpaka sasa Jumla ya wanachama wenye kadi halali ni 87. Ni mategemeo yetu kuwa Ongezeko hilo litazidi kadri ya siku zinavyozidi kuongezeka kwani Mikakati ya kuongeza idadi ya wanachama Imekamilika.

(4)   Kwa Kuwa wanachama wa Tawi hili wengi ni Vijana na wasomi, na kwa kupitia Jumuiya ya vijana Tawi chini ya Mwenyekiti Makini na Mchapakazi asiyeyumbishwa: Bwana Bakunda Chrispin, Tawi limefanikiwa kuwa na mahusiano ya Karibu na Uongozi wa Juu wa Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Hivyo basi shughuli za Vijana ndani ya Tawi zinafuatiliwa kwa Umakini na Matumaini makubwa  kwani UVCCM ndio chemuchemu ya viongozi wa baadae wa chama na serikali.

(5)   Uongozi wa Tawi  umefanikiwa kudhibiti Nidhamu kwa Viongozi na Wanachama wake, mpaka sasa hakuna Taarifa za  Mmomonyoko wa maadili kwa mwanachama katika maaeneo yanayotuzunguka. Ikigundulika kuna Mianya ya Kuvunjiika kwa Maadili ya Kiongozi au Mwanachama Taratibu za kikatiba na Kimwongozo zitafuatwa katika Kudhibiti Swala hilo.

(6)   Katika hatua za kuwa karibu na wanachama wake ndani ya Tawi, Uongozi  Umeanzisha Mawasiliano yakinifu kupitia kitabu cha uso “facebook” , Mpaka sasa kuna Kurasa Mbili zimezinduliwa : “Chama cha Mapinduzi Moscow” na Jumuiya ya umoja wa vijana wa CCM  Urusi.
Lengo la kurasa hizi ni kupokea maoni na Mapendekezo kuhusu jambo lolote ndani ya CCM, pili kuwa na  Mshikamano baina ya wanachama na Viongozi wa Tawi.


SEHEMU YA III:

MATATIZO.
(A)  Hali ya kisiasa ya Tawi:
Chama cha Mapinduzi katika Tawi letu , kimekuwa mstari wa mbele katika kukuza demokrasia ya Maamuzi ndani ya Tawi, Hili linakwenda sambamba na Uenezaji wa sera za chama kupitia website ya Tawi na pia kupitia Jumuiya ya UVCCM  katika Tawi letu.

Ni vema , ikafahamika kuwa Maswala yote yanayohusu Uendeshaji wa Tawi hutekelezwa kwa vikao halali vya Tawi kwa Mujibu wa katiba , na Maazimio hutekelezwa kulingana na Tafsiri halisi ya Shughuli zenyewe kulingana na maagizo ya Vikao husika.

Aidha, kwa kipindi cha Hivi karibuni, kumekuwa na matatizo kadhaa ya Tafsiri halisi za Taarifa za Tawi na maazimio ya vikao, na kupelekea Upoteshwaji wa dhima za Taarifa Husika. Hili linatokana na wanachama kushindwa kufuatilia kwa karibu shughuli za Tawi na CCM na hatimaye kushindwa kutambua Taratibu za kiutendaji na kimaadili ndani ya Tawi kutokana na Utaratibu wa Kimwongozo.

Kwa Ujumla hali ya kisiasa inaendelea kutukuka kutokana na mshikamano wa wanachama na viongozi wanaendesha Gurudumu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa viongozi wa Tawi.
Ni matumaini yangu kuwa amani, ustahimilivu na Busara zetu za kisomi zitatuongoza katika kipindi hiki chote mpaka hapo Viongozi wapya watakapochaguliwa kulingana na Mwongozo wa Uchaguzi Uliopitishwa kwa Kufuata Vikao halali vya Tawi.



(B)   Hali ya Kiuchumi katika Kuimarisha Tawi:
Kwa kuzingatia Taratibu za CCM , hakuna Ruzuku  inayotolewa kwa ajili ya Matawi ya CCM. Matawi yanajiendesha kwa kujitegemea na kutokana na ada za wanachama wa Tawi husika.

Kwa kuzingatia hilo , Nimemuagiza Katibu wa Fedha na Uchumi Pamoja na Idara ya Uchumi na fedha UVCCM , watoe maelezo ya Mapato na Matumizi kwa kipindi chote cha mwaka 2009/2010. Na nini Mikakati  ya Idara zao katika kutafuta Njia za Tawi kujitegemea kiuchumi na Mikakati endelevu ya Baadaye.
Ndugu wanachama, ni Jukumu letu kutambua kuwa Uhai wa Tawi letu kutokana na Malengo yake, uko mikononi mwetu. Ni wajibu wetu kuchangia shughuli za Tawi ikiwemo Malipo ya ada ya Uanachama kwa mwaka 2010/2011 ambayo ni sawa na Rub 4.33 kwa Mwezi.  Taratibu za Malipo na Risiti zitatolewa kupitia idara ya Uchumi na Fedha,

(C)   Upungufu wa Vitabu vya Kisera na Kimkakati vya Chama na Jumuiya. 
Tawi limegubikwa na tatizo hilo kwa kipindi sasa. Kopi za Vitabu ni Chache ukilingana na mahitaji ya wanachama ndani ya Tawi.

 Kutokana na Tatizo hilo, tukiwa katika hatua za kuendelea kuwasiliana na makao makuu Tanzania kwa ajili utumaji wa vitabu zaidi,na vipeperushi vingine:  Nawasihi wanachama wote kufuatilia vitabu vya kisera , Maadili na katiba ya CCM , kwa kupitia link zilizoko kwenye website ya tawi : www.ccmmoscow.blogspot.com.

(D)  Utendaji ndani ya Tawi :
Katika Muda Mfupi Niliokabidiwa madaraka ya Utendaji Mkuu wa Tawi, nimegundua Mapungufu ya Kiutendaji ndani ya Tawi kwa Viongozi na Wajumbe wa halmashauri kuu na wajumbe wa Baraza la kuu la Vijana.

Viongozi na Wajumbe wa Vikao vya halmashauri kuu tunaendekeza Uzembe na kutokuwa Makini kwa kuwa na Mahudhurio mabovu na bila Kujali Muda na thamani ya Uwakilishi wako. Ikumbukwe kuwa uendeshaji wa Tawi unazingatia Maamuzi ya Vikao. Nafikiri  Ili liwe onyo la mwisho, Ikitokea tena Mjumbe /kiongozi hakuudhuria kikao bila kuwa na Taarifa za kimaandishi masaa 24 kabla ya Tarehe tajwa ya Mkutano, utakuwa umeshindwa kutimiza wajibu wako kikatiba  kutokana na dhamana uliokabidhiwa hivyo utakuwa Umejifukuzisha Ujumbe wako!

Ambatanisho na Hilo, Ofisi ya Katibu , inaandaa mkakati wa kupunguza viongozi wa Jumuiya na kuwasilisha hoja katika Vikao vya Tawi kwa ajili ya kujadiliwa,  Jumuiya ambazo zinaonekana zinalega lega na haziwajibiki ipasavyo zitaondolewa katika safu za viongozi wa Tawi. Ni heri kuwa na Viongozi wachache na ambao ni Wachapa kazi.

Nachukua Fursa hii, kwa namna ya kipekee kuupongeza Uongozi na Baraza kuu la UVCCM ndani ya tawi letu kwa kuonyesha umakini wa kiutendaji, kwani Umoja huo ndio Nguzo ya Tawi letu. Nalipongeza Baraza la Vijana la UVCCM kwa kutoa mawazo ambayo ni changamato katika Maazimio ya vikao vya Tawi.



SEHEMU YA IV: 

MATARAJIO NA MIKAKATI YA BAADAE YA TAWI:

(A)Upatikanaji wa Alama za Chama (tshirt, kofia, picha , Vitabu vya Kisekta na kisera )

 Tawi limejiwekea mkakati endelevuwa upatikanaji wa vifaa vyenye ishara ya kutangaza chama na sera   
 zake. Maombi ya Upataikanaji wa vifaa hivyo yatatekelezwa kuanzia Mwaka huu kwa watakao kwenda               Nyumbani.
Pili , kuendelea na Juhudi za Upatikanaji wa vitabu zaidi vya Uelimishaji kisera, pamoja na Majarida mbalimbali yahusiyo CCM.

 Ni matumaini yangu kuwa , Tunapoelekea katika Uchaguzi mkuu wa Tawi, kutakuwa na Mabadiliko        Makubwa , Nawahaidi kama Kiongozi mwenye dhamana ya Utendaji mkuu wa Tawi , Nitalisimamia    kikamilifu na kwa Moyo wangu wote.

(B) Mikakati ya Kiuchumi:

  Kwa Kuzingatia Umuhimu wa Uendeshaji wa Tawi , katibu wa fedha na Uchumi ,Namuagiza aandae Mkakati yakinifu wa Jinsi gani ya kuwa na mradi wa Tawi amabao wanachama wa CCM watanufaika kwa gharama nafuu,
 Pili Ni vema sasa aendelee na mikakati yake ya Upatikanaji wa Fedha toka kwa Wadau mbalimbali kwa ajili ya kuanzisha mradi huo.  Taarifa za uanzilishi wa Mradi huo uwasilishe katika vikao husika kwa ajili ya Majadiliano, na Taarifa Kutolewa kwa wanachama haraka iwezekanavyo:

(C) Uchaguzi wa Viongozi wa Tawi.

Kwa kuzingatia Maazimio ya Vikao vya Juu Tawi vilivyoketi na Maamuzi kufikiwa kulingana na Mazingira ya Tawi letu na wanachama wote, Utekelezaji wa Uchaguzi wa Viongozi wa Tawi unaanza kutekelezwa mwezi Februari 2011 kwa chaguzi za Mashina yote husika ya Tawi, na Baadae uchaguzi wa Viongozi wakuu , kulingana na Ratiba ya Uchaguzi ilivyoainishwa .

Ni jukumu letu sote, kuhamasishana kuanzia sasa kuelewa Misingi ya Chama  na Mwongozo wa Tawi na Baadae kugombea uongozi katika Muda Muafaka kwa dhamira njema ya kulinda, kusimamia na kutetea katiba ya Chama cha Mapinduzi. Mwongozo wa Uchaguzi wenye Kurasa 10 Umeambatanishwa kwenye website ya  Tawi, Nawasihi mfuatilie kwa Makini ili kufahamu taratibu kulingana na Ratiba.

(D)Uenezaji wa Sera na Ufunguzi wa Mashina Nje ya Moscow:

Ofisi ya katibu Mwenezi na sera , ikishirikana na idara ya Chipukizi na Uhamasishaji  wa Jumuiya Vijana, wataanza ziara  katika Mashina Tajwa ya Tawi kwa lengo  la kutoa Elimu ya chama , na wanachama kupata fursa ya kuifahamu CCM  kwa Ujumla pamoja na ilani zake!

Pili , Uongozi wa tawi , Umepanga Mikakati ya Ufunguzi wa Mashina mapya ya CCM hapa Urusi, ikiwemo Riazani, Varonishi, kazani, Nishznii Goradi, Varonishi N.k amboka kuna wakereketwa wa CCM. Hivyo basi Mchakato wa Uandikishaji wa Majina na kujaza Form umeanza, na mara tu utakapokamilika  zoezi la Ufunguzi wa mashina litafuatwa mara Moja.

Mazoezi yote mawili  nilioyataja awali, yataanza  kutekelezwa 1 JULY –SEPT 2010 . hii ni kutokana na Ratiba na Majukumu ya viongozi wa tawi. Kipindi hicho ni Muhimu kwani ni wakati wa likizo.
Ratiba ya  Ufunguzi na Matembezi hayo, yatatolewa kupitia webste ya Tawi: Nawasihi mjitokeze kwa wingi kuelewa Misingi ya CCM na ilani ya Chama

(E)   Ushiriki wa Wanachama katika Uongozi:

Tawi la CCM Moscow ni imara na linaendesha shughuri zake katika Misingi iliyopangwa kwa kuruhusu Uhuru wa Mawazo kwa wanachama wake..
Ofisi ya Katibu,  (block 9 room 1404A kwa siku za alhamisi, ijumaa na jumamosi kuanzia saa 18:00 hadi 21:00.) itakuwa wazi  kupokea Maoni ya Mwanachama,. Maoni hayo yawe katika Maandishi na wala si Maneno ya kuambiwa .Ofisi ya katibu haitashugulikia Taarifa za kuambiwa au kusikia. Kama Kuna jambo Binafsi, lijengewe hoja na Mapendekezo ya Suruhisho na kuwasilishwa Mapema . Kama mtendaji wa Tawi, nitawasilisha Hoja zako katika Vikao vya Tawi kwa kujadiliwa, kwa maslahi ya Tawi zima.

Pia  kwa kufahamu Mchango wako wa Mawazo, Pia unaweza kutoa Maoni yako kupitia internet kwa email : ccmmoscow@gmail.com  au kupitia Kitabu cha uso “facebook”


SEHEMU YA IV: MAJUMUISHO YA HOJA:

Mheshimiwa Mwenyekiti , Baada ya kueleza Taarifa hiyo ya Tawi Japo kwa Muhtasari, Nigependa kutoa Majumuisho ya Maelezo haya kama ifuatavyo;

Ofisi ya Katibu wa Tawi ilipokea Barua toka kwa wanachama 57 yenye kichwa cha habari “ombi la kuitishwa kwa Mkutano mkuu wa CCM Tawi la Moscow Urusi mnamo tarehe 2/5/2010 , barua ya Tarehe 23/4/2010.

Kwa kuzingatia hilo , na kwa niaba ya Uongozi wa Tawi, napenda kuchukua fursa hii  kuwapongeza kwa hatua hiyo, kwa kufanya hivyo , wanachama hawa wamejitendea haki kikatiba na kimwongozo wa Tawi.

Pamoja na Pongezi hizo, ni vema ieleweke wazi kuwa Tafsiri sahihi ya Tawi hili ni CCM Moscow na wala si CCM katika chuo Fulani. Tawi lina maanisha Mjumuiko wa wanachama wote katika shirikisho la Urusi. Hii ni kutokana na Mwongozo wa tawi hili uliwasilishwa Makao makuu ya CCM huko Nyumbani Mapema mwezi February 2009.

Ndugu wanachama, leo Tunakutana na wanachama wa CCM katika Mojawapo ya Eneo la tawi: na sisi kama Viongozi wenye dhamana tumetii ombi lenu japo kwa kuchelewa, ambapo sababu na ufafanuzi wa kuchelewesha ombi leni kutekelezwa nilizitoa mapema zaidi kupitia Website ya tawi, kulingana na utaratibu wa Kiutendaji. Nashukuru kwa kuvuta subira katika hili.

Naomba ieleweke wazi kuwa , mkutano wa leo unatekeleza ombi la wanachama 57 waliondika barua  yao, na kwa maana ya Taratibu za kimwongozo na kiutendaji, Mkutano mkuu wa wanachama wote katika Tawi utaitishwa na Viongozi wa Tawi kupitia Matayarisho ya Agenda za Mkutano zitazokuwa zimepangwa na Sekretarieti ya Tawi.
Kulingana na Majukumu ya shule Mkutano Mkuu Ni vema kufanyika kipindi cha likizo (July –August).

Ndugu wanachama, na viongozi, napenda sasa kuchukua fursa hii, kutoa ufafanuzi wa Tawi kutokana na hoja zilizoanishwa kwenye barua yenu ili kila mwanachama aelewe kwa umakini:-

HOJA 1:  kupata Taarifa za kiutendajin na maendeleo ya Tawi kwani hatuelewi mwelekeo wa Tawi.

UFAFANUZI WA TAWI:

 Natumai nimeeleweka wazi katika hoja hii, nilipotoa ufafanuzi yakinifu na kwa umakini Tulipotoka, mafanikio na matarajio na mikakati ya Tawi
Mwelekeo wa tawi ni kuwaandaa vijana kuwa makada safi watakao kuwa watiifu kwa chama na serikali. Hii ndio dhamira kuu ya Uanzilishi wa Tawi hili.

HOJA YA 2&3: Kutoa elimu na kujadili haki za kimsingi za wanachama: Kujadili Misingi ya Kidemokrasia na utawala bora, katiba na Mwenendo mzima wa Tawi.

UFAFANUZI WA TAWI:
 Napenda ifahamike wazi kuwa, Asilimia 99% ya wanachama wa tawi hili ni wanafunzi , ambao wana majukumu ya shule. Uongozi wa Tawi, unathamini Majukumu ya wanachama katika mazingira  yaliopo ambao ndio msingi mkubwa wa sisi watanzania kuwepo Urusi.

 Kwa kuzingatia Maazimio ya Halmashauri kuu ya Tawi iliyokutana mnamo 24/3/2010: Ratiba ya kutoa sera na elimu kwa wanachama ni Moja ya Mikakati ya Tawi na Utekelezaji wake umepangiwa kipindi cha July –Sept 2010. Ratiba ya Zoezi hili Itatolewa Mapema kupitia website na kurasa za “Face book”

 Nachukua Nafasi hii kuwaasa Mjitokeze kikamilifu katika zoezi hili kichama, na napenda kusisitiza kuwa Ofisi ya katibu mwenezi wa Tawi na Idara ya Chipukizi na Uhamamsishaji wa UVCCM, itaongoza zoezi hili Makini, Ni matumaini yangu kuwa Mtawapa ushirikiano kamilifu.

HOJA YA 4:  Migogoro ndani ya Uongozi:

UFAFANUZI WA TAWI:
Uongozi wa Tawi ni Imara na wala hauna hata chembe ya migogoro kulingana na Tafsiri ya hoja Yenu. Marumbano ya hoja katika vikao Yasitafsiriwe kuwa ni mgogoro, bali ni chachu ya kuelekea mafanikio ya Maazimio kwani Maazimio hupitishwa kwa Kura.

Uongozi unazingatia Taratibu na kanuni za maadili ya Viongozi na wanachama katika kutekeleza majukumu yake. Uongozi wa Tawi unatekeleza Majukumu yake kwa kufuata Maazimio ya Vikao na Taratibu hufuatwa katika Kurejea maamuzi hayo. Huo ndio Utaratibu wa kimwongozo  na Wala isitafsiriwe vinginevyo.




        
HOJA YA 5: Kutoridhishwa na Tarehe ya Uchaguzi iliyopangwa:

UFAFANUZI WA TAWI:

Mchakato wa Uandaaji wa Mwongozo wa Uchaguzi uliandaliwa kwa kupitia kikao cha sekretarieti ya Tawi na Baadae kujadili kifungu kwa kifungu na kamati ya Siasa ya Tawi, na baadae kuwasilishwa katika Kikao cha halmashauri kuu cha tarehe 27/3/2010, ambapo, Kikao hicho Halali cha Tawi kilipitisha Mwongozo huo, na kuwa Utaratibu rasmi wa Kiutendaji , Katika kikao hicho Bi Neema Charles Kengese alithibitishwa Rasmi kuwa Katibu mpya wa tawi baada ya kuteuliwa na kamati ya Siasa kuziba nafasi hiyo iliyokuwa wazi.

Taarifa za Uchaguzi kwa wanachama wote zilianishwa kupitia website, Tangazo kwa wanachama la tarehe 14/4 2010 ambapo linki ya Mwongozo wote ilianishwa, Pia Ratiba ya Mchakato wa kulekea Uchaguzi huo, ilianishwa katika Ukurasa Husika pamoja na sababu zake.

Uongozi wa Tawi, umetoa Maelekezo hayo kwa madhumuni ya kutoa taratibu zitakazowezesha kufanyika maandalizi mazuri na ya kihistoria yatakaofanikisha Uchaguzi Huo.
 Kwa upande wa Kamati ya siasa na halmashauri kuu , Utekelezaji wa Hoja kuelekea Uchaguzi unaanza Mara moja mapema July 2010 kulingana na ratiba.

Napenda kuchukua nafasi hii kuwataadharisha wanachama wenzangu wa Tawi , kuwa Makini na wale wote wenye dhamira mbaya na maaendeleo ya Tawi, wanaopenda kuona tunashindwa kufikia malengo tuliojiwekea ya kulinda mshikamano wetu,  Nawahakikishia kuwa Mshikamano wetu kama wana CCM ni IMARA, na utadumishw  kwa Umakini na Uadilifu wa Viongozi bora si kwa uenezaji wa Propaganda za Wachache wenye uchu wa Madaraka.

Ndugu wanachama : Katika majukumu haya mazito ya Utendaji niliokabidhiwa kama Mtendaji mkuu wa Tawi, leo natamka wazi kuwa, niko tayari kupokea Mapendekezo na Ushauri wa kimaandishi wa Mwanachama na wala si kwa kikundi ndani ya Tawi: Ushauri huo uzingatie njia za kuliimarisha tawi letu, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni kwa kuitangaza Tanzania huku Ugeneni.  Mapendekezo yako ya Msingi yatawasilishwa katika vikao vya Juu Kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa kuwa Utaratibu wa tawi katika mchakato wa Utekelezaji.

HOJA 6: Mwongozo wa utoaji wa Habari
UFAFANUZI WA TAWI:
Mwongozo wa Utoaji wa Taarifa za utendaji wa Tawi kwa wanachama zinazingatia Mamlaka ya Juu ya Tawi, na wala si mtu Binafsi. Taarifa zote zinazowahusu wanachama wa CCM au Jumuiya zinaratibiwa na Uongozi wa Jumuiya husika kupitia Uthibitisho wa Makatibu wa Jumuiya Hizo.

Napenda ieleweke wazi kuwa hakuna ubabaishaji wa utoaji wa Taarifa  zote za kiutendaji za tawi, Taarifa zote ni Kamili kama zilivyoanishwa katika Tangazo husika.
Napenda kuchukua nafasi hii kuwaasa wanachama wote kufuatilia kwa karibu taarifa zote za Kiutendaji kwa umakini na wala SI kusikia kutoka kwa mtu.





MWISHO;
Kwa Wanachama wote:

Nawashukuru wanachama wote 57 kwa kutambua mamlaka ya Tawi la CCM Moscow , na ndio maana mliweza kuwasilisha Barua yenu. Tukio hilo limeonyesha Nidhamu ya hali ya juu na kukua kwa Maadili ya Mwanachama husika : Nawapongeza kwa hilo.

Lakini, nasikitika kusema kuwa Lugha mliotumia kuwasilisha hoja zenu ilikuwa ya jazba na kulazimisha, Ningependa kunukuu tunahitaji uchaguzi mkuu haraka iwezekanavyo…..na kutoa muda wa wiki moja : baada ya tarehe 2/5/2010, nanukuu …… ifikapo tarehe 9/5/2010 tutaunda kamati yetu na tutaitisha mkutano mkuu wa CCM tawi.   Mwisho wa kunukuu!
Napenda kuchukua nafasi hii kuwakumbusha kuwa Uongozi wa tawi ni Imara na kamwe hautayumbishwa na wapinzani wa vyama vya siasa katika tawi., Uongozi hauendeshwi kwa Vitisho ila unazingatia hoja yakinifu na zenye tija kwa kufuata utaratibu wa CCM na mwongozo wa Tawi letu kulingana na mazingira Tuliopo.

Kwa Viongozi wenzangu na Wajumbe wa Vikao vya Tawi:

Kiongozi au Mjumbe wa vikao vya Tawi atakayegundulika anaeneza Propaganda za Uongo ,chuki  ndani ya tawi, huyo ni Msaliti.

Ni jukumu letu kama Viongozi na Wajumbe wa vikao vya Tawi , kutoa Tafsiri sahihi ya Maazimio ya vikao vya Tawi, na si kueneza Majungu kwa lengo la kujitafutia Umaarufu wa Kisiasa tofauti na lengo letu hapa Urusi kama wasomi na wataalamu wa Baadaye wa nchi yetu changa!

Ieleweke wazi kuwa kiongozi au Mjumbe yeyote atakae gundurika kuwa ni kichocheo cha kuvuruga Ustaarabu wa wanachama , kamwe hatavumiliwa , na katiba ya chama ,kanuni za maadili na Mwongozo wa Tawi zitafuatwa na kuondolewa katika safu ya Uongozi  au uanachama wa CCM

Kwa Namna nyingine, Mjumbe au kiongozi anayeona kashindwa kutekeleza Misingi ya Tawi na chama kwa ujumla, Atumie haki yake ya kikatiba kuachia Ngazi. Kwa yeyote mwenye dhamira hiyo, mlango uko wazi na awasilishe barua yake ya kujiuzuru kwa katibu wa Tawi,

Mwishoo kabisa:  Nachukua nafasi hii , kuwaasa watanzania  wenzangu na wana CCM  kuendelea kudumisha umoja na mshikamano wetu , kupendana na kusaidia sisi kwa sisi katika matatizo ya kila mmoja wetu. Kuweka nadharia yenye lengo moja ya kuleta mabadiliko kule nyumbani Tanzania na wala si huku Ugenini.
Nawasihi , Tujikite zaidi katika Taaluma zetu ili kufanya Vizuri kimasomo na  kuitangaza vizuri Tanzania.
Rai yangu kwenu , ni Tushirikiane pamoja katika kusimamia na kutekeleza  majukumu haya mazito niliokabididhiwa na Halmashauri kuu kama Mtendaji mkuu wa Tawi, na nina hakika NITAYAMUDU , kwani Ninajiamini kiutendaji.
Aksanteni kwa umakini wa Kunisiliza! Naamini Tuko pamoja katika Majukumu haya!

Kidumu chama cha mapinduzi:
Bi Neema Charles Kengese:                                                                          22nd May 2010.
Katibu-Tawi la CCM MOSCOW

No comments: