CHAMA CHA MAPINDUZI
UMOJA NI USHINDI, AMANI NA MAENDELEO ...!!!

Wednesday, July 27, 2011

Wabunge waikaanga Wizara ya Kilimo

MBUNGE wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela (CCM), ameikomalia Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, akiitaka iwatendee haki wakulima wa mahindi kwa kuwaacha wauze nje ya nchi. Akichangia makadirio ya wizara hiyo kwa mwaka 2011/2012, Anne alisema serikali haipaswi kuwazuia wakulima kuuza mazao yao, kwa kuwa nao ni wafanyabiashara ambao wanalenga kunufaika na kazi wanayoifanya. Mbunge huyo alisema serikali haina budi kubeba jukumu la kuwatumikia wananchi kwa kuhakikisha hawafi njaa, lakini iwaache wauze mazao wanayoyatolea jasho jingi shambani ili yawanufaishe. "Bei ya mazao ili imnufaishe mkulima lazima izidi gharama anazotumia lakini serikali haimsaidii kuondokana na maradhi, ujinga na umasikini kama Katiba inavyotaka," alisema. Alisema bila kilimo bora na imara nchi haiwezi kusogea na kutaja vipaumbele vinavyotakiwa kufanikisha mpango huo kuwa pembejeo, mbolea, mbegu bora na bei nzuri ya mazao.

Mbunge wa Nkasi Kusini, Desderius Mipata (CCM), aliiomba serikali ifungue mipaka ili wakulima waendelee kuuza mazao yao. "Hawa watu masikini kweli waacheni wauze mazao tena nje ya nchi. Mnapotubana kuuza mazao yetu mnataka nini? Tafuteni njia nyingine kunusuru maeneo ya njaa. Sikubaliani hata kidogo na ninyi kutufungia mipaka," alisema.

Innocent Kalogeris (Morogoro Kusini-CCM), aliiomba serikali ishughulikie vurugu kati ya wakulima na wafugaji, kwa kuwa zinaweza kusababisha vifo iwapo zitaachwa. Alisema wafugaji ndio kikwazo cha mafanikio ya kilimo na wamekuwa wakirudisha nyuma juhudi za serikali kuufanya mkoa wa Morogoro kuwa ghala la taifa la chakula. Naye Lediana Mng'ong'o (Viti Maalumu-CCM), alihoji wakulima wanaozunguka maeneo ya ziwa Victoria na Nyasa kutowezeshwa na serikali ili waondokane na kilio cha mara kwa mara cha njaa.

Kwa upande wake, mbunge wa Mpanda Vijijini, Moshi Kakoso (CCM), alitaka serikali iwathamini zaidi maofisa ushirika walioko wilayani na kuwataka wakurugenzi watendaji wa halmashauri kuacha kuwafanya kama watendaji wa ziada wasiokuwa na umuhimu. "Wakurugenzi hawawathamini, ukienda huko wanawaweka karibu na choo… pembejeo za ruzuku nazo haziwanufaishi wakulima, zinachakachuliwa na huko kwetu (Mpanda) pembezoni zinakwenda hadi Rwanda na kwingineko," alisema. Anna Abdallah (Viti Maalumu -CCM), alisema mbolea inapatikana kwa njia za magendo kutokana na serikali kuacha kuwasaidia wakulima wa korosho. Mbunge huyo alisema hakuna pembejeo za korosho kwa mikoa yote inayolima zao hilo, jambo linalosababisha mfuko mmoja wa mbolea aina ya sulphur kuuzwa sh. 50,000. "Bodi ya Korosho ilimaliza muda wake tangu mwaka 2005 ni nani anayesimamia suala la korosho?" alihoji.

Alisema kutokana na kumaliza muda wake, amekuwa akisikia wajumbe wa bodi hiyo huitwa kujadili mambo yanayojitokeza, ilhali uhalali wao umepitwa na wakati. Mbunge huyo aliomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) akague matumizi ya fedha zinazopelekwa kwa bodi hiyo. Kwa upande wake, Livingstone Lusinde (Mtera -CCM), alihoji kuendelea kutaja kilimo kuwa uti wa mgongo wa taifa wakati watendaji ni tatizo. Alisema watendaji hao wameshindwa kukibadili kilimo katika vitendo na kubaki wakihubiri na kuzungumza mambo ya kwenye makabrasha, ambayo hayana nafasi kwa sasa.

Akizungumzia kilimo, Lusinde alisema wakulima wanafanya kazi katika mazingira magumu, lakini hawana msaada wa maana wa kuwafanya waondokane na kilimo cha jembe la mkono. Mbunge Ally Keissy (Nkasi Kaskazini -CCM), alisema ni ndoto kufikia mafaniko ya kilimo wakati wakulima wanazuiwa kuuza mazao yao nje ya nchi. Alisema wakulima wa Rukwa wameahidi kuwapiga mawe wabunge wa mkoa huo kwa kuwa serikali imewazuia kuuza mahindi yao nje, wakati ambapo imeshindwa kuyanunua yote. Kuhusu vocha za ruzuku kwa wakulima, alisema utaratibu huo umegubikwa na ufisadi na kuufananisha na EPA nyingine kwa madai kuwa, wao kama wabunge wa Rukwa hawazitaki kwa kuwa usimamizi wake ni mbaya.

SOURCE: gazeti la UHURU. Junne 26/7/11

No comments: