Jaji Warioba alisema tangu nchi ipate uhuru mwaka 1961, yamekuwepo mafanikio mengi, miongoni mwa hayo ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa mwaka 1964. Alisema Muungano ni wa wananchi wenyewe na hautegemei orodha ya mambo ya Muungano, ambayo ni masuala ya kiserikali zaidi.
“Huu Muungano unazungumzwa sana, je, hatujaona mafanikio kwa wananchi? Mwananchi hategemei orodha ya mambo ya Muungano,” alisema. Alisema Watanzania wamekuwa wakishirikiana katika masuala mengi na kuzitumia fursa zinazopatikana katika sehemu zote za Muungano, kama biashara na elimu pasipo hata kujua iwapo mambo hayo ni ya Muungano au la. “Muungano huu umefanikiwa kuwaunganisha wananchi, hauoni wakigombana, serikali ndizo zinavutana. Tujiulize, hivi Muungano tunazungumzia wananchi au tunazungumzia serikali,” alihoji Jaji Warioba. Alisema Muungano unapozungumzwa ulenge maslahi ya wananchi na si ya madaraka. “Tusije tukafikiri hatutakuwa na matatizo ya Muungano lakini dira ya kuyatatua ina muhusishaje mwananchi,” alihoji Jaji Warioba na kuongeza kwamba, penye mafanikio pana matatizo pia.
Alionya kuwa, demokrasia ya vyama vingi iwe chachu ya kupata mawazo mbadala na si chanzo cha kuligawa taifa kwa misingi ya ukabila, dini na rangi. “Tusipoangalia vyama vimekuwa kama makabila, wafuasi wanaanza kubaguana,” alisema na kuongeza kwamba, dalili za hali hiyo zimeanza kuonekana katika misiba ya viongozi wa vyama vya siasa. “Hili linaniogopesha, msiba unaanza kuwa mtaji wa kisiasa. Umoja wa nchi hii ni jambo la kitaifa,” alisema. Alisema viongozi wa zamani walikuwa si wasomi sana kama wa sasa, ambao ni wa ‘doti com’ lakini walihakikisha umoja wa taifa unalindwa kwa kutambua umuhimu wake.
Jaji Warioba alisema tangu nchi ipate uhuru, yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta mbalimbali, ikiwemo ya elimu, hivyo kuwa na wasomi wengi, sekta ya afya imekuwa na vituo vingi, na ujenzi wa barabara. Katika hatua nyingine, Jaji Warioba alisema viongozi wa kisiasa wa kuchaguliwa wanapaswa kuondolewa madarakani na wananchi waliowachagua, na si vyama. “Hawa wanaochaguliwa na wananchi hivi madaraka yao yako kwenye vyama vya siasa au madaraka yako kwa wananchi,” alihoji Jaji Warioba na kufafanua kwamba, kwa vile ni viongozi wa kuchaguliwa, wenye mamlaka ya kuwaondoa madarakani ni wananchi.
Ingawa hakutaja chama, lakini mgogoro unaoendelea kwa sasa ambao unaoana na hoja ya Jaji Warioba ni ule wa madiwani wa CHADEMA katika Halmashauri ya Jiji la Arusha, dhidi ya viongozi wa juu wa chama hicho. Uongozi wa juu wa chama hicho unawataka madiwani hao kutohudhuria vikao vya baraza la madiwani na wale wenye nyadhifa katika halmashauri hiyo kujiuzulu, la sivyo watafukuzwa katika chama. Madiwani hao wamekataa kutii maelekezo ya viongozi hao, wakisema wamechaguliwa na wananchi, hivyo waachwe wawatumikie kama walivyowaahidi
No comments:
Post a Comment