CHAMA CHA MAPINDUZI
UMOJA NI USHINDI, AMANI NA MAENDELEO ...!!!

Monday, August 1, 2011

TAMKO LA MKUTANO WA KAMATI KUU YA CCM DODOMA:- 1/8/2011

Mwenyekiti wa CCM Rais Dr.Jakaya Mrisho Kikwete akiongoza kikao cha Kamati kuu ya Halmashauri kuu ya CCM mjini Dodoma leo asubuhi.Wengine katika picha kutoka kushoto ni wajumbe wa kamati hiyo Rais mstaafu awamu ya pili Mzee Ali Hassan Mwinyi,Rais Wa Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar Dr.Ali Mohamed Shein, Rais Mstaafu wa Zanzibar Amani Abeid Karume.Wengine katika picha ni katibu mkuu wa CCM Wilson Mkama na makamu wa CCM bara Pius MsekwaKamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imemaliza kikao chake cha siku moja usiku wa tarehe 31/07/2011 mjini Dodoma chini ya uenyekiti wa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete. Pamoja na mambo mengine Kamati Kuu imeamua yafuatayo;

1. Imefanya uteuzi wa makatibu ishirini na saba (27) kujaza nafasi zilizokuwa wazi katika wilaya hizo. (majina na wilaya zao yameambatanishwa). Pamoja na uteuzi huo, Kamati Kuu imetengua uteuzi wa Makatibu wa Wilaya watatu (3) katika kuboresha ufanisi wa kazi katika wilaya hizo.(majina na wilaya zao yameambatanishwa).


2. Kamati Kuu imepokea na kuridhia taarifa ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kuwakilisha Mkoa wa Tabora, Ndugu Rostam Aziz. Aidha imempongeza kwa uamuzi huo uliozingatia maslahi mapana ya chama chake.


3. Kamati Kuu imepokea pia taarifa ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Ndugu Rostam Aziz na kuagiza chama kupanga ratiba ya mchakato wa kumpata mgombea ubunge wa Jimbo la Igunga itakayozingatia ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi juu ya uteuzi wa mgombea.
Aidha Kamati Kuu imeagiza shughuli zote za kampeni kutafanywa na CCM Mkoa, Wilaya na ngazi zote za chama wilayani Igunga. CCM Taifa watashiriki kuongeza nguvu. Chama kinatoa wito kwa wana CCM, wapenzi na wakereketwa wa chama chetu kushiriki kwa pamoja kuhakikisha jimbo linabaki kwa CCM.

4. Kamati Kuu haijaridhishwa na kiwango cha bei ya mafuta ya taa nchini kwa kuwa ndio nishati inayotumiwa na wananchi wengi wenye kipato cha chini. Aidha Kamati Kuu haikuridhishwa na maelezo ya kupandishwa kwa bei ya mafuta hayo kwa kisingizo cha kuzuia uchakachuaji wa mafuta mengine. Hivyo basi, Kamati Kuu imeiagiza Serikali kutafuta njia za kushusha bei ya mafuta ya taa na kuvitaka vyombo vya Serikali vinavyohusika na usimamiaji wa ubora wa mafuta, vihakikishe vinatimiza wajibu wake kuzuia kabisa mtindo wa uchakachuaji wa mafuta nchini na si kupandisha bei ya mafuta ya taa kama suluhisho.

5. Kamati Kuu inasikitishwa na tatizo la umeme nchini kwani athari zake kwa uchumi wa Taifa na mtu mmoja mmoja ni kubwa. Hivyo basi imeitaka Serikali kutumia muda iliyopewa wa kurekebisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kuja na mpango wa dharura wa kunusuru hali hii na kisha kulimaliza kabisa tatizo la umeme nchini.

6. Aidha Kamati Kuu imejadili masuala mengine kama; migogoro ya ardhi, tatizo la bei ya pamba, tatizo la uuzaji wa mahindi, migogoro migodini, masuala yanayohusu kero za Muungano na kuagiza Serikali kuyashughulikia kwani yanatatulika.


7. Kamati Kuu imeipongeza Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa kwa kazi nzuri ya kutekeleza maamuzi ya NEC na kuitaka iongeze kasi katika utekelezaji huo, ili kuhakikisha mageuzi yaliyokusudiwa yanatekelezwa kwa wakati. Aidha imejadili na kupitisha miundo mipya ya Idara ya Itikadi na Uenezi na Idara ya Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa.

8. Kuhusu suala la maadili ndani ya Chama, Chama kinaendelea kusimamia maadili, na kuwataka wale waliotakiwa kujipima na kuwajibika watumie muda huo, kujipima na kuwajibika kwa masilahi mapana ya chama.
Aidha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa inatarajiwa kukutana wakati wowote mwezi Septemba, ambapo pamoja na mambo mengine itatathimini utekelezaji wa maamuzi yake.
Imetolewa na:-
Nape M. Nnauye (MNEC)
KATIBU WA NEC, ITIKADI NA UENEZI
DODOMA
1/8/2011

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

No comments: