Ndugu Godfrey Zambi, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mbeya na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika;
Ndugu Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM Taifa;
Ndugu Wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa;
Ndugu Makatibu wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa Mliopo;
Watendaji Wakuu wa Serikali na Viongozi wa CCM wa Ngazi Mbalimbali;
Wanachama Wenzangu wa CCM;Mabibi na Mabwana;
Ndugu Wananchi;
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kukutana siku ya leo hapa Mbeya, kuadhimisha miaka 37 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi. Nawashukuru sana viongozi, wanaCCM na wakazi wote wa Mbeya kwa mapokezi mazuri na ukarimu wenu kwangu na wageni wenzangu tangu tulipowasili jijini hapa jana mpaka sasa. Hakika tutaondoka Mbeya tukiwa na kumbukumbu nzuri ya ukarimu na upendo wenu kwetu.
Shukrani nyingine nazitoa kwa viongozi na wanachama wenzetu wa Mbeya kwa kukubali kuwa mwenyeji wa sherehe hizi. Nafahamu fika kwamba kuandaa sherehe kubwa kama hii si jambo jepesi. Lakini, inafurahisha na kuleta faraja kwamba, kutokana na moyo wenu wa kujitolea, umahiri na umakini wenu, mambo yamefana sana. Matembezi ya mshikamano yalifana sana na hapa kiwanjani mambo ni mazuri sana. Hongereni sana.
Niruhusuni, kupitia hadhara hii, niwapongeze kwa dhati viongozi, wanachama, makada, wapenzi na washabiki wote wa CCM kote nchini kwa kuadhimisha miaka 37 ya uhai wa Chama chetu. Tunafanya sherehe hizi leo kwa vile tarehe 5 Februari, 2014 ni siku ya kazi. Si vyema kuwatoa watu kazini. Ndiyo maana tunafanya madhimisho haya leo. Tunayo kila sababu ya kusherehekea siku hii kwa vifijo na nderemo kama tufanyavyo siku zote. Hii ni kutokana na ukweli kuwa CCM ina historia iliyotukuka, kuvutia na kusisimua. Chama chetu kimepata mafanikio makubwa tangu kuasisiwa kwake tarehe 5 Februari, 1977 mpaka sasa. Tumefanya mambo mengi mazuri kwa maslahi ya nchi yetu na watu wake. Nchi imetulia, kuna amani na utulivu na maendeleo ya kichumi na kijamii yanazidi kupatikana kila kukicha. Mwenye macho haambiwi tazama.
Ni jambo linalofurahisha na kutia moyo na, la kujipongeza kwa kipindi cha miaka 37 kati ya hiyo 22 ikiwa ndani ya mfumo wa vyama vingi, CCM imeendelea kuwa Chama kikubwa na chenye nguvu kuliko vyama vyote hapa nchini. Aidha, CCM imebaki kuwa chama chenye mafanikio makubwa na kukubalika zaidi na Watanzania kuliko vyote kwa kila hali na kwa vigezo vyote. Wapo wanaojaribu kuiga lakini hawajaweza. Kwa kweli, itawachukua miaka mingi kufikia hata theluthi moja ya hapa tulipofikia sisi. CCM inaongoza na wengine wanafuatia.
Ninyi na mini tunavifahamu vyama kadhaa vya siasa ambavyo vilianzishwa lakini havijapata mafanikio kama Chama chetu na baadhi havikudumu. Baadhi ya vyama na watu walijifanya bundi na kukitabiria kifo Chama cha Mapinduzi. Nilisema wakati ule kuwa CCM haifi na si ajabu vitakufa vyama vyao na CCM wataiacha hapa hapa. Haya kiko wapi? CCM ipo haipo? CCM hai siyo hai? CCM ipo, CCM ni hai na wala haina dalili ya ugonjwa wo wote. Wahenga walisema dua la kuku halimpati mwewe na mchimba shimo hujichimbia mwenyewe. Baadhi yao sasa wanahangaika nchi nzima wakitapatapa kujinusuru. Wanakabiliwa na migogoro mikubwa inayotishia uhai wao. Lakini, sisi hatuwaombei mabaya.
Kuimarisha Chama
Ndugu Viongozi;
WanaCCM Wenzangu;
Pamoja na ukweli kwamba Chama cha Mapinduzi ni kikubwa, kina nguvu na kimepata mafaniko makubwa tusije tukalewa mafanikio na kujisahau hata mara moja. Wenzetu wanaendelea kujijenga na wanapata mafanikio ya kiasi chao. Hivyo basi, lazima tuendelee kufanya kazi ya kuimarisha Chama ili kiendelee na hata kizidi kukua na kuwa na nguvu kubwa zaidi. Mtakumbuka kuwa, Oktoba, 2006 tulianzsha Mradi wa Kuimarisha Chama kwa lengo la kuelekeza na kuongoza shughuli ya kuimarisha Chama cha Mapinduzi. Huu ni mradi wa tatu katika historia ya CCM. Lazima tufanye kila tuwezalo kuhakikisha kuwa malengo na madhumuni ya Mradi huo yanatekelezwa kwa ukamilifu. Hatuna budi kutambua kuwa uhai na maendeleo ya CCM sasa na kwa miaka mingi ijayo yatategemea ufanisi wetu katika utekelezaji wa Mradi wa Tatu wa Kuimarisha Chama.
Ndugu Viongozi na WanaCCM;
Kwa sababu ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani kazi ya kuimarisha Chama cha Mapinduzi ina umuhimu wa kipekee. Lazima tupate mafanikio katika jambo hilo kwani yanakipa Chama chetu nguvu ya kutuwezesha kupambana na kupata ushindi katika chaguzi hizo. Kazi nzuri tuliyofanya katika utekelezaji wa mradi wa kuimarisha Chama miaka iliyopita ndiyo iliyotupa mafanikio makubwa ya 2009 na 2010 tunayojivunia sasa. Hivyo basi tukifanya vizuri mwaka huu tutapata ushindi kama ule au hata zaidi.
Bila shaka sote tunatambua kuwa kazi ya kuimarisha Chama inahusisha mambo matatu: Kwanza, kujenga na kuimarisha Chama kama taasisi. Pili kufanya kazi ya Chama ndani ya umma. Na tatu ni kufanya kazi ya kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama, sera na maamuzi ya Chama unaofanywa na Serikali na vyombo vyake. Naamini wote mnajua kuwa sizungumzii mambo mapya. Mambo yote matatu tunayajua kwani tumekuwa tunayafanya kwa miaka mingi. Ninachokifanya leo ni kukumbushana juu ya umuhimu wa kuendelea kufanya kazi hiyo ila tuifanye kwa ufanisi zaidi, kwa nguvu zaidi, ari zaidi na kasi zaidi.
Viongozi Wenzangu na Wanachama Wenzangu;
Bahati nzuri mwezi Novemba, 2012 tulikamilisha Uchaguzi ndani ya Chama, hivyo tunayo safu mpya madhubuti ya viongozi wa Chama chetu na Jumuiya zake ya kuongoza mpaka mwaka 2017. Kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, viongozi hao ndiyo watu wenye jukumu la kihistoria la kuongoza CCM na wanachama wake kutafuta na kupata ushindi katika chaguzi zijazo mwaka huu na mwaka ujao. Hivyo basi, viongozi tuliochaguliwa hatuna budi kuitambua dhamana hiyo kubwa tuliyopewa na wanachama wenzetu. Lazima kuhakikisha kuwa tunatimiza ipasavyo wajibu wetu huo. Tusiwaangushe wanachama wenzetu. Kwa ajili hiyo lazima tujipange vizuri, tuelekeze akili zetu, nguvu zetu na muda wetu kwenye kuhakikisha kuwa Chama cha Mapinduzi kina uwezo na sifa ya kukiwezesha kupata ushindi mnono.
Ndugu Viongozi Wenzangu;
Jambo la kwanza muhimu kwetu kufanya ni kuona kuwa viungo vyote vya Chama chetu viko kamilifu na vinafanya kazi vizuri. Chama kiwe na wanachama wengi ambao wanatimiza ipasavyo wajibu wao kwa Chama chao. Viongozi wa Chama wawe hodari kufanya kazi ndani ya Chama na ndani ya umma. Wasiwe mangimeza bali watoke waende kwa wanachama kuimarisha uhai wa Chama. Waende kwa wananchi kukisemea Chama, kusikiliza shida zao na kusaidia kutafuta ufumbuzi. Lazima Chama kiwe mlezi na kimbilio la wananchi. Tukifanya hivyo watu wetu watakuwa na imani na mapenzi na CCM hivyo watakiunga mkono katika chaguzi za dola. Tuhakikishe kuwa vikao vinafanyika ipasavyo kwani vikao ndiyo msingi mkuu wa demokrasia ndani ya Chama. Maamuzi ya Chama hufanywa na vikao siyo kiongozi peke yake. Lazima pia Chama kiwe na uwezo wa rasilimali fedha na vifaa ili viongozi na wanachama waweze kufanya kwa ufanisi kazi ya Chama ndani ya Chama na nje ya Chama na ndani ya umma.
Napenda kutumia nafasi hii kuwakumbusha agizo letu la siku nyingi la kila ngazi ya Chama kuwa na shughuli za kuwaingizia mapato na kuw ana Mfuko wa Uchaguzi. Bado maagizo haya hayajatekelezwa ipasavyo kote nchini. Uhodari wa uongozi hupimwa kwenye matatizo. Lazima viongozi wa CCM tuwe wabunifu ili tulipatie jawabu endelevu, tatizo la ukwasi hasi. Tatizo linalohatarisha murua wa Chama cha Mapinduzi kwani baadhi ya viongozi na wanachama sasa hawachagui nani anachangia Chama. Tunachukua hata mtu mwenye pesa chafu au wenye nia chafu. Hata wanaotoa rushwa nao hupokewa kishujaa badala ya kuwanyanyapaa na kuwaweka mbali nasi.
Jambo lingine muhimu kuhusu kuimarisha CCM kama taaasisi ni kuwa na Jumuiya zilizo imara ili kukiongezea Chama wanachama, wapenzi na washabiki wa kukiunga mkono wakati wote na hasa wakati wa uchaguzi. Jambo la mwisho kubwa na muhimu ni kuwepo umoja na mshikamano miongoni mwa viongozi kwa viongozi, wanachama kwa wanachama na baina ya viongozi na wanachama. Hii ndiyo silaha ya kuangamiza adui na kujihakikishia ushindi. Unapokosekana umoja na mshikamano, adui hupata nafasi ya kupenya. Ndiyo maana wakati mwingine hata pale tusipostahili kushindwa tunashindwa. Hivyo tuzingatie na kutekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya CCM ya Umoja ni Ushindi.
Ndugu Viongozi na Ndugu Wanachama;
Uwezo na sifa ya Chama cha Mapinduzi kupata ushindi kunategemea pia taswira yake katika jamii. Kama taswira yake ni nzuri Chama hukubalika kwa watu hivyo wanakuwa tayari kukiunga mkono. Kama taswira ya Chama ni mbaya watu hukichukia na hukataa kukiunga mkono. Katika mazingira hayo kushindwa huwa ni dhahiri. Ili mpate ushindi mnalazimika kufanya kazi ya ziada na kutumia nguvu kubwa mno. Aghalabu, ushindi wenyewe huwa mwembamba. Sera nzuri za CCM, utendaji mzuri wa Serikali zake na matendo mema na tabia njema za viongozi na wanaCCM hujenga mapenzi ya jamii kwa Chama na hivyo kuungwa mkono. Sera mbaya, utekelezaji mbaya wa Serikali, vitendo vya rushwa, wizi na ubadhilifu huondoa mapenzi ya wananchi kwa Chama. Huzaa chuki na hupunguza kuungwa mkono na kuhatarisha ushindi. Lazima wakati wote tuhakikishe kuwa taswira ya Chama chetu mbele za watu ni nzuri. Watu wote na mambo yote ambayo yatakuwa kinyume yashughulikiwe ipasavyo tena kwa wakati muafaka. Ajizi nyumba ya njaa. Usipoziba ufa utajenga ukuta.
Ndugu Zangu, WanaCCM Wenzangu;
Nawasihi sana tulipe uzito unaostahili suala la uadilifu wa viongozi wetu na wanachama. Bila ya hivyo Chama kinaweza kuwa imara na Serikali yake ikatekeleza majukumu yake ipasavyo, lakini kikakosa kuungwa mkono na kupoteza ushindi kwa sababu ya tabia na mwenendo usiofaa wa viongozi na wanachama. Ndiyo maana Chama kikaunda Kamati za Usalama na Maadili kufanya kazi ya kuwabana wanaokiuka maadili. Naomba Kamati hizo zifanye kazi zake ipasavyo. Kutokufanya hivyo kunaathiri sana hadhira ya kukubalika kwa CCM katika jamii. Hususan nawataka tufanye kila linalowezekana tuondokane na tabia ya kutoa na kupokea rushwa katika kuchagua viongozi na mchakato wa uteuzi wa wagombea.
Tusikubali uovu huu ikageuka kuwa mila na desturi ndani ya Chama kikubwa na chenye historia iliyotukuka kama CCM. Vitendo hivi lazima tuvikatae na tuvipige vita kwa nguvu zetu zote. Tusiwaache watu wachache wanaotaka uongozi kwa gharama yo yote waharibu sifa nzuri ya Chama cha Mapinduzi. Tusiache ikajengeka dhana potofu kwamba ukitaka uongozi ndani ya Chama uwe kupitia CCM na uwezo wa kifedha kuhonga watu ndani ya Chama na nje ya Chama. Tusikubali kuacha Chama chetu kifikishwe hapo. Tunakitoa thamani mbele ya watu na kuhatarisha uhai wake. Tuchukue hatua stahiki sasa kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Maadili za Chama chetu. Wale wote wanaofanya vitendo hivyo na mawakala wao wadhibitiwe.
Ndugu Zangu;
Viongozi Wenzangu na WanaCCM Wenzangu;
Kama nilivyokwishadokeza awali, kuimarisha Chama cha Mapinduzi ni pamoja na kufanya kazi ya Chama ndani ya umma. Viongozi wa Chama lazima watoke kwenda kuwatembelea wananchi, kuzungumza nao, kuona au hata kushiriki katika shughuli zao. Kuwajulia hali na kutambua faraja zao na matatizo yao. Yaliyo mema yaimarishwe na matatizo yapatiwe ufumbuzi. Bahati nzuri CCM ndiyo yenye Serikali, hivyo viongozi wakiyakuta matatizo na kutoa taarifa kwa mamlaka za Serikali katika ngazi husika yatashughulikiwa.
Sina budi kumpongeza sana Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Abdulrahman Kinana kwa kuonesha njia na kutoa mfano kuhusu kufanya kazi ya Chama ndani ya umma. Katika ziara zake Mikoani akifuatana na baadhi ya Makatibu wa Sekretarieti na viongozi wengine wa CCM amekuwa anafanya kazi kubwa na nzuri sana. Ziara zake zinakijenga Chama cha Mapinduzi na kutoa taswira nzuri ya Chama chetu katika jamii. Zinahuisha uhai wa CCM. Ndugu Kinana amekuwa anafanya mambo ambayo hayajazoeleka kufanywa. Ametembelea maeneo ambayo si viongozi wengi hufika. Wakati mwingine amekuwa anatumia njia za usafiri zinazoogopesha wengi. Hukaa na wananchi, anakula nao na kufanya kazi nao. Na kubwa zaidi amekuwa anatoa fursa kwa wananchi kuelezea matatizo yanayowasibu, manungu’uniko yao na kero zao.
Bahati nzuri Katibu Mkuu pia, amekuwa anashiriki katika kutafuta majawabu ya matatizo anayoambiwa. Hii imesaidia sana kumaliza baadhi ya matatizo kulekule mikoani. Pale ambapo pamekuwa panahitaji hatua zaidi za Serikali hakusita kutoa taarifa kwa Waziri Mkuu. Vilevile amekuwa anatoa taarifa ya ziara zake kwenye Kamati Kuu ya CCM. Pale ilipoonekana kuna haja kwa viongozi na watendaji wakuu husika kuitwa kwenye Chama ilifanyika hivyo. Matatizo yalizungumzwa na kutafutiwa ufumbuzi.
Ndugu Wananchi;
Mfano mzuri ni pale Mawaziri wangu wanne walipoitwa na Kamati Kuu baada ya ziara ya Mkoa wa Ruvuma na Mbeya. Matatizo yahusuyo sekta zao yalizungumzwa na uamuzi kufanywa kuhusu hatua za kuchukuliwa. Najua wapo watu, walitaka Mawaziri hao wafukuzwe kazi. Kwa vile halikufanyika basi likageuzwa kuwa suala la malumbano. Napenda ieleweke kuwa kuitwa Kamati Kuu hakuna maana ya kuishia kufukuzwa. Wameitwa kwa sababu ya kuwepo matatizo yaliyoonekana yanatakiwa yapatiwe ufumbuzi. Matatizo yamezungumzwa na maelekezo kutolewa kuhusu cha kufanya. Kamati Kuu imetimiza wajibu wake uliobaki ni wa Serikali. Kamati Kuu itaendelea kufuatilia na kama hakuna maendeleo ndipo inapoweza kuamua kuomba mamlaka ya uteuzi ichukue hatua zipasazo dhidi ya mhusika. Hatujafika huko.
Hongera Ndugu Kinana kwa kusimamia na kutekeleza kwa vitendo maazimio ya Mkutano Mkuu wa Chama chetu. Napenda kutumia hii fursa kutoa wito kwa viongozi wote wa Chama na ngazi zote kuiga mfano huu mzuri. Ongezeni nguvu na jitihada maradufu katika kufanya kazi ya siasa ndani ya umma. Sisemi haifanyiki, lakini tuongeze nguvu.
Viongozi Wenzangu na Wanachama Wenzangu;
Nawaomba muendelee kuyasemea mambo mazuri yaliyofanywa na yanayoendelea kufanywa na Serikali ya CCM. Muendelee kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM unaofanywa na Serikali na pale kwenye matatizo muyatambue na kuyatafutia ufumbuzi. Wakati huo huo fuatilieni ahadi zilizotolewa na viongozi wetu ambazo hazijatekelezwa ili zitekelezwe. Muda uliobaki ni mfupi, hivyo tuongeze kasi. Hatutaki ifikapo 2015 wananchi watunyooshee vidole vya lawama na kutusuta. Namna pekee ya kuepuka kusutwa ni kutimiza ahadi zetu kama tulivyoahidi. Pale tutakaposhindwa kukamilisha tuwe wazi na kutoa sababu za kushindwa kwetu na mipango ya kutekeleza. Ili tuweze kusimamia utekelezaji wa Ilani vizuri, viongozi tuzidi kujielimisha kuhusu Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Tujue kwa undani inazungumzia nini na kisha tuwafuatilie viongozi na watendaji wa Serikali waitekeleze.
Ndugu Wananchi;
Kwa jumla utekelezaji wa Ilani na Sera za CCM na ahadi za Serikali unaenda vizuri. Si yote yamekamilika na kwamba huenda tusiyamalize yote tuliyokusudia kuyafanya. Hiyo haitatokana na uzembe au kupuuzia bali kwa sababu ya kutopata fedha zote tunazohitaji. Kimsingi mambo mengi mazuri yameyafanyika na tunaendelea kuyafanya. Katika maeneo yote kuna mafanikio ya wazi kwa kila mtu kuona. Iwe kwenye elimu, maji, afya, barabara, umeme na mengineyo.
Kwa upande wa elimu, kwa mfano, tumepanua sana nafasi za masomo kwa vijana wetu katika ngazi zote kuanzia elimu ya msingi hadi vyuo vya juu. Upanuzi huo umewezesha watoto na vijana wetu wengi kupata fursa ya kupata elimu na mafunzo. Kazi tunayofanya sasa kwa nguvu na ari kubwa ni kuboresha elimu inayotolewa. Tunachofanya sasa ni kuhakikisha walimu wapo wa kutosha na kila shule zinakuwa na vitabu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinavyokidhi mahitaji. Hii ni pamoja na kuhakikisha kila shule inakuwa na maabara za sayansi. Vilevile, tunaboresha mazingira ya walimu ya kuishi na kufanyia kazi. Kazi hizo tunaendelea nazo vizuri.
Ndugu Wananchi;
Maji nayo tumeyapa umuhimu wa juu katika utekelezaji wa malengo ya Ilani na Sera za Serikali. Lengo letu kuu ni kuona kuwa asilimia 90 ya watu wa mijini na asilimia 65 ya watu wa vijijini wanapata maji safi na salama ifikapo 2015. Kama fedha zitapatikana kama ilivyopangwa tunatarajia kuwa katika mwaka 2013/14 watu milioni 7.1 watapata maji. Katika mwaka ujao wa fedha 2014/15 tumepanga kuwapatia maji watu wengine milioni 7 na mwaka utaofuata (2015/16) tutaongeza tena huduma hiyo kwa watu milioni 1.3. Hatua
hizo zinatufanya tufikie malengo kwa miji ambayo ni zaidi ya lengo.
Mafanikio pia yapo katika kuboresha upatikanaji wa huduma ya afya kwa wananchi wa Tanzania. Zahanati, vituo vya afya na hospitali zimeendelea kujengwa kote nchini. Aidha, hospitali za wilaya, mikoa, kanda na Hospitali ya Taifa Muhimbili zimeendelea kuboreshwa. Kwa ajili hiyo idadi ya Watanzania wanaoweza kupata huduma ya afya iliyo bora inazidi kuongezeka. Hali kadhalika, wataalamu wa afya wa fani mbalimbali wameongezeka na hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba imezidi kuboreshwa.
Tumeendelea na jitihada za kuboresha miundombinu ya barabara, reli na umeme. Kwa upande wa barabara lengo letu la kuunganisha mikoa kwa barabara za lami linaendelea vizuri. Mwaka jana tulikamilisha ujenzi wa kilometa 877 za barabara za lami na ujenzi wa nyingine unaendelea sehemu mbalimbali nchini. Kuhusu reli, tunaendelea kuimarisha reli ya TAZARA na reli ya kati ili ziweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Mchakato wa kuboresha njia ya reli na ununuzi wa mabehewa na injini unaendelea vizuri. Kwa upande wa TAZARA ni matumaini yetu kuwa masuala ya uendeshaji yatapatiwa ufumbuzi na Serikali za nchi zetu mbili.
Aidha, jitihada zetu za kuwapatia umeme Watanzania kwa asilimia 30 ifikapo 2015 zinaendelea vizuri. Tumefanikiwa kuongeza idadi ya Watanzania wanaopata umeme kutoka asilimia 10 mwaka 2015 hadi asilimia 24 mwaka 2013. Kwa kasi tunayoendelea nayo hivi sasa, naamini tutavuka lengo letu hilo. Haya yote ni mafanikio ya kujivunia.
Ndugu wananchi;
Kwa hapa Mkoani Mbeya, nawapongeza kwa kupiga hatua nzuri ya maendeleo katika maeneo mbalimbali. Kwa upande wa elimu mmefanikiwa kupanua fursa za elimu katika ngazo zote. Mkoa unao shule za msingi 1,094 zenye wanafunzi 532,765, shule za sekondari ni 310 zenye wanafunzi 152,289; vyuo vikuu 3 na matawi kadhaa ya vyuo vikuu pamoja na vyuo 6 vya ualimu. Kazi mliyonayo ni kuwasimamia na kuwaongoza vijana wetu watumie ipasavyo fursa hizo.
Kwa upande wa afya, upanuzi wa Hospitali ya Mkoa unaendelea vizuri na majengo ya hospitali pamoja na wodi yanaendelea kujengwa. Katika mwaka wa fedha 2013/2014 zaidi ya shilingi milioni 300 zimetengwa kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa wodi ya watoto na Mkandarasi wa kuifanya kazi hiyo tayari ameshapatikana. Suala la ghala la MSD ndani ya hospitali tutalipatia ufumbuzi mapema iwezekanavyo.
Ndugu Wananchi;
Kuhusu maji, kwa mwaka 2013/2014 miradi 80 ya maji inatekelezwa katika vijiji 112 ambapo kati ya hiyo miradi 15 imekamilika. Miradi hiyo ni Namkukwe (Chunya), Namtambalala (Momba), Masoko (Kyela), Kyimo (Rungwe), Mbambo, Kipapa na Kikuba (Busokelo), Ubaruku na Chimala (Mbarali), Mbebe na Luswisi (Ileje), Ikombe (Kyela), Maninga (Mbozi), Iwalanje na Shongo/Igale (Mbeya). Aidha, miradi mingine 55 iko katika hatua mbalimbali za ujenzi na mingine 10 iko katika hatua za zabuni. Jumla ya shilingi bilioni 38.14 zinategemewa kutumika katika ujenzi wa miradi hiyo itakayohudumia watu wapatao 508,064. Itakapokamilika itafanya huduma ya maji vijijini kufikia asilimia 73.5. Kwa hapa mjini nafahamu hali ya upatikanaji wa maji safi na salama inaridhisha. Ombi langu kwenu, tunzeni vyanzo vya maji ili upatikanaji wa maji uwe wa uhakika.
Kwa upande wa umeme, kuna miradi 12 ya umeme vijijini ambayo inatekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA). Miradi hii imeshakamilika kwa asilimia 94 katika Wilaya za Mbeya Vijijini miradi minne, Mbozi miradi mitatu, Chunya miradi mitatu na Rungwe miradi mwili. Miradi hii imegharimu jumla ya Shilingi billioni 7.6 na wateja wanaendelea kuunganishwa. Katika mwaka 2014, jumla ya vijiji 170 vitapatiwa umeme na jumla ya shilingi bilioni 82.26 zimetengwa kwa madhumuni hayo. Mradi wa umeme wa Matema Wilayani Kyela, ambao ni ahadi yangu sasa umekamilika na umeme unasambazwa kwa wananchi. Katika Jiji la Mbeya kuna miradi ya umeme chini ya mpango wa utekelezaji wa Millenium Challenge Account Tanzania (MCA-T) ambayo imekamilika kwa asilimia 99.
Barabara ya Mbeya - Chunya inaendelea kujengwa (Rift Valley- Lwanjilo imekamilika kwa asilimia 25 na Lwanjilo – Chunya imekamilika kwa asilimia 78). Kasi ya ujenzi ni ndogo hasa kwa kipande cha Mbeya – Lwanjilo kwa sababu ya mkandarasi wa kwanza kushindwa kazi. Naamini Wizara itachukua hatua stahiki kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara hiyo. Ujenzi wa barabara ya Kyela hadi Matema Beach umeanza na mwaka huu kasi itaongezwa kwa kuanza mchakato wa kujenga kilometa 18. Usanifu wa barabara ya Mpemba –Isongole umekamilika kitakachofuata ni kutafuta fedha za ujenzi. Tunazitafuta. Hivyo ndivyo ilivyo kwa barabara ya Mpemba – Itumba na barabara ya Katumba – Ruangwa – Tukuyu. Kwa upande mwingine inatia moyo kuona kuwa sasa barabara nyingi zaidi za vijijini zinapitika mwaka mzima.
Ndugu Wananchi;
Aidha, ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Songwe umekamilika kwa asilimia 95 na kuwezesha ndege kutua. Ujenzi wa jengo jipya la abiria unaendelea na unategemewa kukamilika miezi miwili ijayo. Kazi za kuweka tabaka la mwisho la zege kwenye maegesho ya magari, kununua na kufunga lifti na ngazi ya umeme zinaendelea. Hata hivyo ili mazao ya kilimo yaweze kusafirishwa, tumewashauri Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania wajenge ghala kwa ajili ya mazao yanayoharibika haraka. Pia wafunge taa kwenye njia
ya kutua na kuruka ndege.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa kilimo napenda kutoa pongezi kwa Mkoa wa Mbeya kuendelea kuwa ghala la chakula la kutumainiwa. Naomna mwaka huu mvua ni nzuri hivyo endeleeni kudumisha kazi nzuri muifanyayo. Tutaendelea kuwaunga mkono na hasa kwa upande wa kurahisisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo. Inatia moyo kuona mengi tulioahidi katika Ilani za 2005 na 2010 tumeyatekeleza na mengine tunaendelea kuyatekeleza. Naomba viongozi mueleze mafanikio hayo yaliyopatikana. Kazi hii siyo ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu na viongozi wengine wa kitaifa peke yao. Ni kazi ya viongozi wote waliopo katika ngazi mbalimbali za uongozi kuanzia kwenye Shina. Naomba tuifanye kwa bidii, bila kuchoka.
Kwenye kuifanya kazi hiyo, hakuna kulala. Yapo mambo mengi mazuri ya kusema na hakuna mwingine wa kuyasemea zaidi yetu sisi wenyewe. Tusiposema sisi wananchi waliotutuma hawatafahamu tuliyowafanyia na wakati mwingine watapotoshwa na watu wasiotutakia mema. Ni kazi inayotakiwa kufanywa na kila kiongozi wa CCM na wanachama wao pia. Kufanya hivyo tutatambuliwa na kuheshimiwa inavyostahiki. Tukifanya hayo sioni kwa nini CCM isiendelee kushika dola kwa miongo mingi ijayo.
Mchakato wa Katiba
Ndugu WanaCCM;
Mchakato wa Katiba Mpya unakwenda vizuri mpaka sasa. Tarehe 30 Desemba, 2013 nilipokea Rasimu ya Pili ya KatibaMpya na Taarifa ya Tume ya Katiba. Taarifa ya Tume imekusanya maoni ya wananchi kuhusu mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kero zao, mapendekezo ya marekebisho ya sera mbalimbali na mambo mengi yanayohusu maisha yao. Serikali itayatafakari mapendekezo hayo nakuchukua hatua zipasazo. Rasimu ya Katiba itafikishwa katika Bunge la Katiba ambalo tunategemea litakutana katika wiki ya tatu ya mwezi huu. Bunge litaijadili Rasimu na kuamua watakavyoona inafaa. Mwishoni mwa mjadala Bunge Maalum litakuwa limetupatia Rasimu ya Mwisho ya Katiba ambayo itafikishwa kwa wananchi kwa uamuzi kupitia Kura ya Maoni.
Ndugu Wananchi;
Kinachosubiriwa kwa hamu hivi sasa ni uteuzi wa Wajumbe 201 wa Bunge Maalum la Katiba na kutangazwa kwa siku ya Bunge hilo kuanza. Kazi ya uteuzi wa Wajumbe imefikia ukiongoni naamini ndani ya siku mbili zijazo orodha hiyo itatangazwa. Lazima nikiri kuwa ilikuwa kazi ngumu sana. Waombaji ni wengi mno ukilinganisha na nafasi zilizopo. Tumejitahidi kwa kadiri ya uwezo wetu kupata uwakilishi mpana kwa mujibu wa sheria. Hivyo tunajua watakuwepo watu wengi waliotumaini kupata wao au watu waliotaka wao wateuliwe lakini hawakufanikiwa.
Kuhusu siku ya kuanza nina imani kwa wiki ya tatu ya mwezi Februari, 2014 Bunge hilo linaweza kuanza. Nayasema hayo baada ya kutembelea ukumbi wa Bunge Dodoma na kuelezwa maendeleo ya maandalizi ya ukumbi, majengo mengi muhimu na vifaa vya kuwezesha kikao cha Bunge kufanyika. Nimeelezwa kuwa tarehe 10 Februari, 2014 matengenezo ya ukumbi yatakuwa yamekamilika na majaribio ya vipaza sauti yatafanyika siku hiyo kuthibitisha ubora wake. Kwa maoni yangu muda usiozidi siku 5 – 7 baada ya siku hiyo utatosha. Ndani ya siku mbili zijazo tunaweza pia kutangaza siku ya Bunge kuanza.
Ndugu Viongozi, WanaCCM na Wananchi Wenzangu;
Ni matumaini yangu kuwa Wajumbe watafanya kazi yao kwa umakini na uadilifu ili kuipatia nchi yetu Katiba nzuri inayotekelezeka, itakayoimarisha Muungano badala ya kuudhoofosha. Katiba itakayodumisha amani na utulivu nchini na kuongeza zaidi kasi ya kuleta maendeleo. Najua muundo wa Muungano litakuwa ndilo suala litakaloleta mvutano katika Bunge Maalum la Katiba. Kutakuwa na mjadala mkali kuhusu upi muundo bora, Muungano wa Serikali mbili kama ilivyo sasa au Muungano wa Serikali tatu unaopendekezwa kwenye Rasimu ya Katiba.
Ni matumaini yangu kuwa kila upande utatumia hoja zenye nguvu kushawishi na kufanikiwa kuungwa mkono na upande wa pili. Nimesikitishwa na kauli ya Mwenyekiti wa CHADEMA Mheshimiwa Freeman Mbowe kuwa watatumia hata ngumi kupata kukubaliwa kwa mfumo wa Serikali tatu. Sijui ni kukosa ukomavu wa kisiasa au ni kitu gani. Jambo la wengi utalilazimishaje kwa ngumi. Jawabu ni kujenga hoja zenye mashiko na kwa umahiri mkubwa ili wenzako wakuelewe na kukubalia. Kutumia nguvu hakutasaidia na wala siyo njia bora ya kutunga Katiba. Napenda kutumia nafasi hii kumkumbusha Mheshimiwa Mbowe kutambua kuwa ugomvi Bungeni hautaleta jawabu bali kuvuruga mambo. Siamini kuwa mambo kuvurugika kuna maslahi yoyote kwake. Ugomvi haujengi bali unabomoa.
Ndugu Wananchi;
Niliwahi kuelezea rai yangu kwa vyama vya siasa kukutana kuzungumzia namna bora ya kushirikiana na mahusiano wakati na baada ya Bunge kuanza na kumaliza kazi yake. Nilitoa rai ile kwa kuamini kuwa ushindani na mivutano baina ya vyama unaweza kukwamisha mambo. Bahati nzuri baada ya mashauriano, vyama vya siasa nchini vimekubaliana kukutana wakati wowote wiki ijayo. Kwa kweli, hii ni hatua muhimu sana ya maendeleo. Inaanza kuleta matumaini ya mchakato huu kuanza na kuisha kwa salama na amani.
Ndugu Viongozi na Wanachama Wenzangu;
Mwisho napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza sana wenyeji wetu wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa na wale wote walioshiriki kuandaa sherehe hizi ambazo zimefana sana. Nawashukuru pia wanachama na washabiki, wakereketwa na wapenzi wa CCM pamoja na wananchi wa Mbeya kwa kujitokeza kwa wingi kuja kujumuika katika kilele cha sherehe hizi hapa uwanjani, Asanteni sana kwa mapenzi yenu makubwa kwa Chama cha Mapinduzi.
Naomba viongozi wenzangu maadhimisho haya yawe kichocheo cha kuwatumikia wananchi kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi. Wanatupenda, wanatuamini na wanatuthamini. Twendeni tukawatumikie, tusiwaangushe.
Kidumu Chama cha Mapinduzi!
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment